Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulio haramu ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa, hujuma hizo zimefichua sura halisi ya Wamagharibi likija suala la haki za binadamu.
Vasily Nebenzia amesema hayo katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, “Israel imefanya hujuma mara chungu nzima nchini Syria, likiwemo shambulio dhidi ya uwanja wa ndege wa Damascus mwezi Juni, baada ya kupata ridhaa ya Washington.”
Ameeleza bayana kuwa, Israel inakanyaga misingi na sheria zote za kimataifa kwa mashambulizi hayo, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa hususan nchi za Magharibi ambazo zimeridhia kuendelea hujuma hizo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amesisitiza kuwa, “Tunalaani vikali kuendelea kwa mashambulizi ya anga ya Vikosi vya Anga vya Israel dhidi ya maeneo mbalimbali ya Syria.”
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alilalamikia mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria, na kuitaka Washington iheshimu haki ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu. Alisema, Umoja wa Mataifa una wasiwasi kutokana na mashambulio kama hayo hasa kwa kuzingatia hali tete iliyopo kwenye eneo hili.
Mashambulizi ya kijinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani nchini Syria yamekuwepo tangu miaka kadhaa nyuma tangu ulipoundwa muungano eti wa kimataifa wa kukabiliana na magaidi wa Daesh (ISIS).