Russia: Tutazipiga na chini sarafu za dola na euro kwa kushirikiana na waitifaki wetu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, Moscow inaimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na nchi marafiki zake na kwamba ina uhakika kwa ushirikiano huo itaweza kuziangusha sarafu za dola na euro kwani sarafu hizo ni sumu.

Kwa mujibu wa ripoti ya leo Jumamosi ya shirika la habari la IRNA, Alexander Pankin amesema hayo alipohojiwa na shirika la habari la TASS na kuongeza kuwa, Moscow inahitaji kuwa na mfumo salama wa mabadilishano ya fedha ambao si SWIFT na hivi sasa Benki Kuu ya Russia inaandaa mfumo wa kubadilishana  data za kifedha uitwao SPFS ambao utakuwa na uwezo wa kupambana na mashinikizo ya kigeni.

Amesema, ijapokuwa uamuzi wa kuwa na mfumo mpya wa mabadilishano ya fedha haukufanywa na Russia kwa hiari, bali baada ya kulazimika kufanya hivyo kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi, lakini ni mfumo madhubuti ambao unaweza kukabiliana vilivyo na ule wa SWIFT.

Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa SWIFT wa mabadilishano ya fedha kimataifa na jinsi ulivyotengenezwa ili kuzifanya nchi zote ziifuate na ziinufaishe Marekani na Magharibi kutaka na kukataa na kuongeza kuwa, mfumo huo wa SWIFT umetengenezwa kwa ajili ya dunia inayotawaliwa na kambi moja na hauwezi kukidhi haja ya dunia inayotawaliwa na kambi kadhaa.

Amma kuhusu ukiritimba wa sarafu za dola na euro katika miamala yote ya kifedha ya kimataifa duniani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, Moscow ina waitifaki wenye uchumi imara na ana uhakika kuwa, kwa kushirikiana na waitifaki wake hao wanaweza kuzipiga na chini na kuziweka pembeni sarafu za dola na euro katika miamala yao ya kimataifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *