Russia na China zimeulaani vikali utawala wa Israel kutokana na utumiaji wake mabavu kupita kiasi dhidi ya Wapalestina huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Palestina, siku ya Jumatatu, naibu balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyanskiy aliulaani utawala wa Israel kwa “utumiaji nguvu kupita kiasi” katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Vile vile ameonya kwamba “hatua za upande mmoja” za utawala huo zikiwemo za upanuzi wa vitongoji, kunyakua mali ya Wapalestina, kubomoa nyumba zinazomilikiwa na Wapalestina, kutiwa mbaroni kiholela na kukiuka hali ya sasa ya maeneo matakatifu ya al-Quds kunaendelea kubadilisha ukweli wa mambo.”
Polyanskiy amebainisha zaidi kuwa “vitendo haramu vya kiholela vya utawala haramu wa Israel haviishii tu katika mipaka ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza bali vinaathiri mataifa jirani ya Kiarabu, ambayo mamlaka yao ya kujitawala yanakiukwa mara kwa mara”, akimaanisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria na Lebanon.
Balozi huyo pia ameikosoa Marekani, mshirika mkuu wa Israel, kwa kupinga mara kwa mara maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Israel na Palestina.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Zhang Jun, pia ameeleza kuwa nchi yake ina “wasiwasi mkubwa” kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Akizungumzia mwaka 2022 kuwa mwaka mbaya zaidi kwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi tangu 2005, Zhang amesema Beijing inalaani “mashambulio yote ya kiholela dhidi ya raia, inachukizwa na ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto, inapinga vikosi vya usalama vinavyotumia nguvu kupita kiasi na inatoa wito kuwajibishwa wahusika.”
Balozi huyo pia amezungumzia hali mbaya ya kibinadamu na kiuchumi katika Ukanda wa Gaza, akiitaka Israel kuondoa vikwazo vyake vya miaka 15 kwenye eneo hilo la pwani.
Zhang amehimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa “kuwaunga mkono watu wa Palestina katika kurejesha na kutekeleza haki zao zisizoweza kuondolewa.” Aidha amesema, “Katika masuala yanayohusu mustakabali na hatima ya watu wa Palestina, hakuna mtu aliye na haki ya veto.”
Hivi karibuni vikosi vya Israel vimekuwa vikiendesha mashambulizi na mauaji ya kila siku katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hasa katika miji ya Jenin na Nablus, ambako makundi mapya ya wapiganaji wa muqawama wa Palestina yameundwa.