Wizara ya Ulinzi wa Russia imesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimefanikiwa kudhibiti kikamilifu mji wa kistratajia wa Soledar, ulioko katika eneo la Donbass. Eneo la Donbass lenye raia wenye asili ya Russia liko mashariki mwa Ukraine na tangu 2014 Warusi walianzisha jamhuri mbili, Donetsk na Luhansk, na kuunda serikali zilizojitenga na serikali ya Ukraine.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Wizara ya Ulinzi wa Russia imeeleza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kutwaa kikamilifu mji huo wa kimkakati wenye utajiri wa madini ya chumvi, kwa kushirikiana na askari wa shirika binafsi la kijeshi la Wagner.
Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, kudhibitiwa kwa mji huo kutawapa fursa wanajeshi wa Russia kukabiliana barabara na askari wa Ukraine, katika mji mkubwa zaidi wa Bakhmut unaopakana na mji huo wa Soledar.
Televisheni ya Russia imewaonyesha wanajeshi wa nchi hiyo wakiwa wanashangilia ushindi huo muhimu baada ya jeshi la Russia kuwatimua askari wa Ukraine na kuudhibiti mji huo baada ya operesheni ya angani na nchi kavu.
Nchi za Magharibi zinazorundika silaha na zana za kijeshi nchini Ukraine zimeingiwa na wahaka na kiwewe kufuatia ushindi wa Russia katika operesheni yake ya kijeshi ya Russia katika mji huo ulioko Donbass nchini Ukraine.
Tarehe 24 Februari mwaka uliomalizika 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia alitoa amri ya kuanza operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo hilo la Donbass, akijibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa Marais wa Jamhuri za Donetsk na Luhansk.
Hatua hiyo ya Putin ilichukuliwa sanjari na maombi ya mara kwa mara ya Ukraine ya kujiunga na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) na baada ya nchi hiyo kupokea msaada wa mamilioni ya dola kutoka nchi za Magharibi.