Balozi wa Russia nchini Marekani anasema “vitendo visivyokubalika” vya jeshi la Marekani karibu na ardhi ya Russia ni “sababu ya wasiwasi,” huku akiitaka Washington kusimamisha safari “za ndege za uhasama” karibu na mipaka ya nchi hiyo.
Anatoly Antonov alisema hayo katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Telegram siku ya Jumatano, siku moja baada ya Moscow kusema kuwa ilinasa ndege isiyo na rubani (droni) ya MQ-9 ya Marekani juu ya maji ya Bahari Nyeusi.
Balozi huyo amesema: “Tunachukulia kwamba Marekani itajiepusha na uvumi zaidi katika vyombo vya habari na kusimamisha safari za ndege karibu na mipaka ya Russia,”na kuongeza kuwa, “Hatua yoyote ya ya Marekani kutumia silaha ni uhasama waziwazi.”
Aidha amesema Moscow inafahamu vyema kwamba droni hizo za Marekani katika mipaka ya Russia zinakusanya data kwa maslahi ya wanajeshi wa Ukraine kwa ajili ya kukabiliana na wanajeshi wa Russia.
Mwanadiplomasia amesema ana uhakika kwamba iwapo ndege isiyo na rubani ya Russia itatokea karibu na maeneo ya Marekani, “jeshi la Marekani litachukua hatua kali na halitaruhusu anga yake au eneo la maji kuvurugwa.”
Antonov pia alisema Washington tayari imeipatia Kiev silaha zenye thamani ya dola bilioni 33, akibainisha kuwa, “Ni wazi kabisa kwamba ni Marekani ambayo inachochea kwa makusudi mzozo wa Ukraine moja kwa moja kwa silaha.”
Jeshi la Marekani limedai kuwa ndege ya kivita ya Russia ilinasa propela ya ndege moja ya kijasusi isiyo na rubani ya nchi hiyo na kuifanya ianguke kwenye Bahari Nyeusi jana Jumanne katika makabiliano ya kwanza ya moja kwa moja kati ya madola hayo mawili tangu Russia ilipoanzisha operesheni za kijeshi nchini Ukraine mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo Wizara ya Ulinzi ya Russia imekanusha kuwa ndege yake ya kivita iligongana na ndege hiyo isiyo na rubani (UAV) na kubainisha kuwa, droni hiyo ya Marekani ilianguka baada ya kufanya kile ilichokiita “upindaji wa ghafla”. Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Russia imeongeza kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani iligunduliwa karibu na peninsula ya Crimea, ambayo Moscow iliiunganisha na shirikisho la Russia kutoka Ukraine mwaka 2014.