Russia yapeleka manowari 3 za kubebea makombora Bahari Nyeusi

Russia imepeleka manowari tatu za kubebea makombora katika Bahari Nyeusi na kuziweka meli hizo za kivita katika hali ya tahadhari.

Duru za habari zinaarifu kuwa, manowari hizo za kijeshi zimesheheni makombora 20 aina ya Kalibr. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Russia,  Sergei Shoigu, kombora moja la Kalibr linaweza kubeba kichwa cha nyuklia chenye uzani wa kilo 500.

Waziri huyo amesema bayana kuwa, kombora hilo la Kalibr lina uwezo wa kupiga shabaha umbali wa kilomita 1,500 kwa usahihi mkubwa.

Russia imeonya mara kadhaa kuwa, Uingereza na Marekani zinafanya njama za kuanzisha mzozo na vita katika Bahari Nyeusi, lakini Moscow italinda mipaka yake kwa kutumia njia zote za kidiplomasia, kisiasa na kijeshi. Hii ni baada ya manowari ya kivita ya Uingereza kuingia bila ya ruhusa katika maji ya Russia kwenye visiwa vya Crimea.

Haya yanajiri siku chache baada ya Marekani kutangaza kuiongezea Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 1.85 ikiwa ni pamoja na kuipelekea Ukraine mfumo wa makombora wa Patriot.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Haungari, Viktor Orban amesema suala la kuendelea na kumalizika vita nchini Ukraine lipo mikononi mwa Marekani.

Amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Magyar Nemzet na kuongeza kuwa, “Ukraine inaweza kupigana tu madhali inaendele kupata uungaji mkono wa fedha na silaha kutoka Marekani. Iwapo Wamarekani wanataka amani, bila shaka itapatikana.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *