Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesisitiza kuwa Moscow inazingatia kikamilifu pendekezo la kuhamisha makao makuu ya Umoja wa Mataifa kutoka Marekani hadi sehemu nyingine.
Alexey Drobinin, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: “Katika miaka ya mwanzo mwa kuasisiwa Umoja wa Mataifa, wakati pande zote zilikubali kwamba makao makuu ya Umoja wa Mataifa yatakuwa New York, Marekani ilichukua majukumu ya nchi mwenyeji na kutia saini makubaliano husika na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.”
Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa: “Sasa, Marekani inakwepa kutekeleza makubaliano haya kama nchi mwenyeji na haitekelezi wajibu wake wa kuwa mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa.”
Alexey Drobinin pia amesema kuwa hivi sasa Russia inatatizika kupata viza kwa ajili ya wajumbe wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa huko New York, wakati Merekani inalazimika kutoa viza bila kuchelewa na bila masharti.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa Russia, sio Moscow pekee inayokabiliwa na matatizo hayo, bali nchi nyingine ambazo Marekani inaziona kuwa nchi mahasimu wake zinakabiliwa na vikwazo na matatizo kama hayo kwa ajili ya kuhudhuria kwenye vikao vya Umoja wa Mataifa mjini New York.