Rais William Ruto amelegeza msimamo wake kuhusu vita kati ya Israel na Palestina, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 27,000.
Kupitia kwenye simu mnamo Alhamisi, Februari 1, Ruto alizungumza na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kuhusiana na vita katika Ukanda wa Gaza ambapo aliibua wasiwasi kuhusu mzozo wa kibinadamu.
“Nimeelezea wasiwasi wa Kenya juu ya hali inayozidi kuzorota huko Gaza ambapo upotezaji wa maisha umefikia viwango visivyokubalika,” Ruto alibainisha.
Aidha alisisitiza haja ya mataifa hayo mawili kutatua masuala yanayotokana na vita na kutetea amani kwa ajili ya maelfu ya familia zilizoathirika.
“Nilisisitiza imani ya Kenya katika suluhu ya serikali mbili ambayo ingeruhusu kuwepo kwa amani bega kwa bega kwa mataifa ya Israel na Palestina,” alibainisha.
Rais pia alitarajia kwamba vita hivyo, ambavyo vimevutia hisia za kimataifa na kusababisha Afrika Kusini kuwasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), vitamalizika.
“Nina matumaini ya kumalizika mara moja kwa mzozo wa Gaza,” Ruto aliongeza.
Rais wa Kenya mnamo Oktoba 8 aliunga mkono Israel, akiitaja Palestina kama magaidi. Aidha alitoa wito kwa wahalifu hao kufikishwa mahakamani, kwani ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
“Kenya inaungana na mataifa mengine duniani katika mshikamano na Taifa la Israel na inalaani bila shaka ugaidi na mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia nchini,” alisema.
Vita vya Israel na Palestina vilivyoanza Oktoba 7 hadi sasa vimegharimu maisha ya zaidi ya watu 27,000, na kuacha 66,139 kujeruhiwa.
Israel iliilaumu Hamas – kundi la wanamgambo wa Palestina, kwa kuandaa vita baada ya kundi hilo kuua watu waliokuwa wakisherehekea katika tamasha la muziki la jangwani la Supernova.
“Watu wa Kenya na serikali yao kwa hili wanatoa pole na kutuma rambirambi kwa familia za waathiriwa wote,” Ruto aliwapa pole walioathiriwa mwezi Oktoba.