Isaac Herzog, rais wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, jana Jumapili tarehe 30 Januari aliwasili mjini Abu Dhabi katika safari ya kwanza rasmi ya kuutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati.
Safari ya Herzog nchini Imarati ni ya kwanza kufanywa na rais wa utawala wa Kizayuni katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kabla ya kuelekea huko, Isaac Herzog alieleza kuwa, anaelekea Umoja wa Falme za Kiarabu kutokana na ombi rasmi alilopata kutoka kwa Mohamed bin Zayed al Nahyan, mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi. Safari hiyo ya rais wa utawala wa Kizayuni nchini Imarati ni mwendelezo wa hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida iliyochukuliwa na pande hizo mbili.
Desemba mwaka 2020, Imarati ilisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Mapatano hayo yalisainiwa Ikulu ya White House na kuhudhuriwa na rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump. Baada ya kusainiwa makubaliano hayo, uhusiano wa tawala hizo mbili umefuata mkondo wa ustawi, ambapo mbali na kufunguliwa balozi katika miji ya Abu Dhabi na Tel Aviv, safari za kidiplomasia baina ya pande mbili zimeongezeka pia.
Nukta ya kutafakari hapa ni kwamba, safari zilizofanywa na viongozi wa Israel nchini Imarati ni nyingi na zimehusisha maafisa wa ngazi ya juu kabisa wa utawala huo haramu. Baada ya safari hii ya Isaac Herzog, ndio kusema kuwa, viongozi wote wakuu wa utawala wa Kizayuni wameshatembelea Abu Dhabi na kufanya mazungumzo na viongozi wa Imarati. Kabla ya rais wa Israel, waziri mkuu Naftali Bennett, waziri wa mambo ya nje Yair Lapid na vilevile mkuu wa shirika la usalama wa ndani Shabak, pamoja na maafisa wengine kadhaa waandamizi wa utawala huo ghasibu, walikuwa tayari wameshaitembelea Imarati. Kupitia safari hizo za kidiplomasia, utawala wa Kizayuni unafuatilia zaidi malengo ya kisiasa na kujaribu kuutumia pia uhusiano wake na Abu Dhabi kama kigezo na mfano wa kuigwa na nchi zingine za Kiarabu.
Safari ya Isaac Herzog imefanyika katika hali ambayo, hivi karibuni mapigano kati ya Imarati na Wayemeni yamepamba moto. Baada ya kuendelea uingiliaji wa Imarati katika vita dhidi ya Yemen, Wayemeni wamechukua hatua mara mbili ya kushambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani miji ya Abu Dhabi na Dubai. Baada ya mashambulio hayo, waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett aliwasiliana na mrithi wa ufalme wa Imarati Mohamed bin Zayed na kumpa pendekezo la Tel Aviv kuipatia Abu Dhabi msaada na uungaji mkono wa kiusalama na kiintelijensia. Kwa hivyo hakuna shaka kuwa msimamo huo wa utawala wa Kizayuni kuisaidia na kuiunga mkono Imarati katika vita dhidi ya Yemen utakuwa umekaririwa na kurudiwa tena katika safari ya rais wa utawala huo mjini Abu Dhabi.
Kwa upande mwingine, safari ya rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Abu Dhabi imefanyika katika hali ambayo, utawala huo dhalimu umekuwa ukishadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina. Sera za uangamizaji kizazi, ujenzi haramu wa vitongoji, mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza na vilevile jinai dhidi ya mateka Wapalestina zingali zinaendelea kwa nguvu, ukatili na kasi ileile. Kuhusiana na hilo, na katika msimamo iliotoa kuhusu safari ya Herzog nchini Imarati, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeeleza katika taarifa kwamba, safari za aina hiyo na kuwakaribisha viongozi wa adui wa Kizayuni katika miji mikuu ya Kiarabu na Kiislamu ni zawadi kwa utawala huo ghasibu na kuushajiisha uendeleze kwa nguvu zaidi jinai zake dhidi ya Wapalestina na kupora zaidi haki zao.
Nukta nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba, safari ya Herzog nchini Imarati imefanyika sambamba na kuendelea mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 4+1 na kujitokeza ishara za kufikiwa mwafaka katika mazungumzo hayo. Utawala wa Kizayuni siku zote umejionyesha kuwa ni mmoja wa wapinzani wakuu wa kufufuliwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Mazungumzo ya Vienna yalikuwa moja ya ajenda za mkutano wa rais wa utawala haramu wa Israel na viongozi wa Imarati. Hata hivyo mazungumzo hayo hayawezi kuwa na taathira yoyote kwa sababu kabla ya hapo, wakati Naftali Bennett alipoelekea Abu Dhabi na kuzungumza na viongozi wa Imarati kuhusu mchakato wa kufufuliwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, mashauriano yao hayakuwa na athari yoyote kwa mchakato huo.
Nukta ya mwisho ni kwamba, wakati wa safari ya Isaac Herzog kuelekea Imarati, ndege iliyombeba mzayuni huyo ilipita kwenye anga ya Saudi Arabia. Picha za tukio hilo zinaonyesha kuwa, Herzog si tu amefurahishwa na suala hilo lakini pia amesema, ana matumaini kwamba karibuni hivi uhusiano wa Saudia na utawala wa Kizayuni utabadilika na pande hizo mbili zitapiga hatua ya kuutangaza rasmi na hadharani uhusiano wao huo../