Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Alkhamisi ya jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Imarati katika safari yake huko Abu Dhabi na kujadiliana naye kuhusu masuala yanayozihusu pande mbili na matukio muhimu zaidi ya kikanda na kimataifa.
Katika mazungumzi hayo, Ali Shamkhani, abaye pia ni mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Kiislamu, ameashiria uhusiano wa siku nyingi wa nchi hizo mbili pamoja na masuala yanayozikutanisha pamoja ya kitamaduni na kidini na kusisitiza ulazima wa kupanuliwa na kuzidishwa uhusiano kati ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu katika nyanja zote.
Kwa upande wake, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Zayed bin Sultan Al Nahyan, ameeleza kuridhishwa kwake na ziara ya Admeri Ali Shamkhani huko Imarati na amepongeza makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Tehran na Riyadh, akiyataja kuwa ni hatua madhubuti katika njia ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano baina ya nchi za kanda hii. Amesema ana matumaini kwamba safari ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran huko Imarati itafungua ukurasa mpya katika mahusiano ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Safari ya Shamkhani katika UAE, pamoja na umuhimu na maana yake ya kimkakati, inaonyesha sura mpya ya diplomasia ya kikanda; na imefanyika chini ya wiki moja baada ya tangazo la kuanzishwa tena uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia tarehe 10 Machi zilikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena ofisi za kibalozi ndani ya kipindi cha miezi miwili. Makubaliano hayo yalifikiwa mjini Beijing chini ya upatanishi wa China.
Sasa baada ya makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia, nchi nyingine za eneo la Ghuba ya Uajemi kama Imarati pia zinajaribu kuboresha uhusiano wao na Iran. Kwa msingi huo, hivi karibuni Imarati ilitoa dhamana kwamba hakuna upande wowote anaoweza kutumia ardhi ya nchi hiyo kwa ajili ya kuishambulia Iran. Ali Shamkhani pia alisema kabla ya safari ya siku moja huko Abu Dhabi kwamba: Mtazamo wa serikali ya sasa ya Iran kuhusu ushirikiano wa kieneo unaofuatiliwa katika fremu ya diplomasia ya ujirani mwema ni kuunda eneo madhubuti la lenye nguvu.
Katika miezi ya hivi karibuni, licha ya kuwepo hitilafu katika nyuga za kisiasa na kikanda, Iran na Imarati zimefanya mikakati ya kuhakikisha kwamba kunakuwepo uhusiano utakaozuia kuongezeka mivutano, na kutumia uwezo uliopo katika nchi hizo mbili hususan katika uga wa biashara na uchumi.
Kuhusiana na suala hili, tangu mwaka jana, Iran na Imarati zilifanya mazungumzo juu ya kuboresha uhusiano kutoka ngazi ya balozi mdogo hadi balozi kamili, na hatimaye Tehran na Abu Dhabi ziliwatambulisha mabalozi wao wapya. Pande hizo mbili pia zilifikia maelewano katika baadhi ya mambo, ikiwa ni pamoja na sekta ya fedha na benki.
Ni wazi kuwa siasa za ujirani mwema na uhusiano wa kirafiki na majirani ni moja ya malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa kuzingatia hayo, Iran hapo awali ilipendekeza “Mpango wa Amani wa Hormuz” kwa lengo la kutatua migogoro na hitilafu zilizopo na baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu za eneo la Ghuba ya Uajemi. Mwaka uliopita pia, Tehran ilizidisha maingiliano ya kisiasa na kiuchumi na nchi hizo, ikifanya juhudi za kutatua au kupunguza tofauti zilizopo na kuzielekeza nchi hizo upande wa kuunda mfumo wa usalama wenye mwelekeo wa ndani bila ya kuingiliwa na mataifa ya kigeni.
Ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi yanayofanana kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ambayo kuimarishwa kwake kunahitaji mshikamano na ushirikiano endelevu. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mazungumzo kati ya nchi za eneo hili ndiyo njia pekee sahihi ya kutatua masuala na mizozo iliyopo bila ya kuingiliwa na nchi ajinabi. Kwa msingi huo, katika kikao chake na Rais wa Imarati, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran ameeleza nafasi ya mambo yanayosababisha migogoro ambayo yanatishia usalama na utulivu wa Ghuba ya Uajemi chini ya uongozi wa nchi za nje ya kanda hiyo na kusisitiza kwamba: Juhudi za kupatikana usalama wa pamoja unaozingatia uwezo wa ndani zinaweza kuwa mwisho wa mingi kati ya migogoro ya sasa.