Faraan ; Seneta Johnson Sakaja anayepingwa kuwania ugavana wa Nairobi kwa madai hana Digirii, Jumatatu alisema alisoma katika Chuo Kikuu cha Teams University na kuhitimu Oktoba 2016.
Katika ushahidi aliowasilisha kwa jopo la Tume ya Uchaguzi (IEBC) la kutatua mizozo ya uteuzi na uidhinishaji wa wawaniaji, Bw Sakaja anayedaiwa hajahitimu kwa shahada hiyo, alidai wamepotoka wala hawana ukweli wowote.
Bw Sakaja anadai alihitimu 2016 lakini ukurasa ulio na jina lake na mahafali wengine haukuwasilishwa kortini na walalamishi wanne wanaopinga kuwania kwake kwa ugavana wa Kaunti ya Nairobi.
Bw Sakaja alisema kesi hizo nne hazina mashiko kisheria na zinapaswa kutupiliwa mbali kisha aruhusiwe kuendelea na kampeni zake.
Pia Sakaja amekana jina lililowasilishwa kortini ambalo ni Sakaja Koskei Johnson.
“Jina lililo katika cheti cha mashtaka si langu. Jina langu halisi ni Sakaja Johnson Arthur,” anasema Sakaja.
Jopo hilo lilielezwa kuwa kesi nne zilizowasilishwa dhidi ya Bw Sakaja zinalenga kumharibia muda ili asishiriki katika kampeni.
Wakati huo huo, mwaniaji kiti cha useneta wa Kaunti ya Kiambu, Bw Paul Karungo Thangw’a kwa tikiti ya chama cha UDA, alieleza jopo la IEBC kwamba hakutimuliwa kazini kama Waziri wa Masuala ya Vijana katika serikali ya Ferdinand Waititu Baba Yao kwa sababu ya ufisadi.
“Bw Thangw’a hakutimuliwa kazini kwa sababu ya ufisadi. Mawaziri wote wa serikali ya Waititu walifutwa kazi, Baba Yao alipofukuzwa ugavana na Seneti,” alisema wakili Ng’ang’a Mbugua.
Bw Mbugua anayemwakilisha Thangw’a alieleza jopo la IEBC linaloongozwa na George Mburugu kuwa mwanasiasa huyo aliendelea kupokea mshahara wa uwaziri wa Sh187,000.
“Mshahara ulilipwa mfanyakazi na wala si mtu aliyetimuliwa kazini,” Bw Mbugua alieleza jopo hilo.
Lakini afisa msimamizi wa uchaguzi katika Kaunti ya Kiambu, Bw Arnold Mutwiri alisema hakumwidhinisha Bw Thangw’a kwa kuwa alipokea ushahidi alitimuliwa kazi kwa sababu ya ufisadi.
Uamuzi iwapo Bw Thangw’a ataidhinishwa au la utatolewa Juni 18,2022.