Samia aweka msimamo uanzishwaji wilaya mpya

Dar/Mbeya. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haina mpango wa kukata maeneo kwa kuyapandisha hadhi, badala yake wanajielekeza kwenye utatuzi wa kero za wananchi.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana mkoani Mbeya, wakati akizindua mradi wa maji wa Shongo – Mbalizi baada ya kupokea ombi kutoka kwa mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza la kutaka Mbalizi kupandishwa hadhi na kuwa halmashauri ya mji.

Mbunge huyo alimwomba Rais Samia kuupandisha hadhi mji huo, ili uwe halmashauri ya mji akidai itasaidia kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi wa Mbalizi na maeneo mengine jirani.

Akizungumzia jambo hilo, Rais Samia alisema alipokea ombi hilo kutoka kwa viongozi, lakini akawaeleza wananchi kwamba Serikali imejielekeza kwenye utatuzi wa kero zao.

“Nilipofika uwanja wa ndege, mkuu wa mkoa na mbunge waliniambia kuhusu halmashauri nikawaambia, halmashauri maana yake ni gharama zaidi, viongozi zaidi, mishahara zaidi, magari zaidi, gharama kwa Serikali, majengo zaidi, gharama kwa Serikali.

“Kwa sasa, wananchi wangu wa Tanzania wana shida chungu nzima, wanataka umeme, wanataka madarasa. Mwaka jana tulijenga madarasa 15,000 ya sekondari na mengi katika shule za msingi.

“Lakini watoto wetu wanafanya mitihani karibuni hapa…mwakani natakiwa niwe na madarasa 8,000 Tanzania nzima. Yatabebwa na Serikali ili msichangishwe, msibughudhiwe, Serikali itafute hiyo pesa ikajenge madarasa,” alisema Rais Samia.

Kiongozi huyo alieleza bado wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi, kama vituo vya afya, madarasa, maji, umeme na barabara, hivyo kwa uwezo wa Serikali haitawezekana kufanya yote kwa wakati mmoja.

“Wananchi mnataka vituo vya afya, mnataka maji. Tukisema tunakatana halmashauri na Tanzania nzima inataka kukatwa maeneo, hatutaweza. Uchumi wetu bado haujaruhusu, acha tumalize shida za wananchi, tukishamaliza tutakwenda kukatana kwenye maeneo.

“Kwa sasa kipaumbele nilichoagizwa na Chama cha Mapinduzi ni shida za wananchi, kwa hiyo hilo la halmashauri litabaki hivyo,” alisema Rais Samia wakati akizungumza na wananchi wa Mbalizi.

Baada ya kuzindua mradi wa maji wa Mbalizi, Rais Samia alifungua jengo la huduma ya mama na mtoto na baadaye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mbeya na aliupongeza mkoa huo kwa kutekeleza kikamilifu miradi hiyo.

“Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya miradi kwenye Serikali za mitaa, nimeridhika na utekelezaji wa miradi ya maji, hospitali na ofisi ya makao makuu ya mkoa.

“Niwape pongezi kwamba pesa inapokuja mnaitumia vema, na hivi ndivyo Mkoa wa Mbeya mmefanya. Niwaambie tu furaha yangu ni kuona ofisi hii ya mkuu wa mkoa wa Mbeya,” alisema Rais Samia.

Aliwataka madiwani katika mkoa huo kwenda kusimamia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri yanayoelekezwa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba fedha hizo zinarejeshwa na wote waliokopeshwa.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga alisema mradi wa maji wa Shongo – Mbalizi uliozinduliwa na Rais Samia utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 8 – 12 na utahudumia wananchi zaidi ya 80,000.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mbeya kutoka asilimia 44 zilizokuwepo kabla ya mradi huo hadi kufikia asilimia 65 za sasa baada ya mradi huo kukamilika,” alisema Sanga.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mbarawa alisema wizara imepokea ombi la wabunge wa Mkoa wa Mbeya la kutaka barabara ya lami ya njia nne iliyopangwa kujengwa kuanzia Igawa hadi Ifisi, iongezwe kilomita mbili ili ifike Uwanja wa Ndege wa Songwe.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *