Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Sana’a amelaani kuzingirwa wananchi wa Yemen na kuitaja hatua hiyo kuwa inazuia kurefushwa muda wa usitishaji vita nchini humo.
Usitishaji vita uliofikiwa kati ya serikali ya Sana’a na muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudia ulianza kutekeleza Aprili Pili; na Hans Grundberg Mjumbe wa Umoja wa Mataifa huko Yemen ametangaza kuwa, oparesheni zote za kijeshi za nchi kavu, anga na baharini zinapasa kusimamishwa kwa mujibu wa mapatano hayo.
Tarehe Pili mwezi Juni Grundberg alisema kuwa, serikali ya Sana’a na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia zimekubaliana kuongeza muda wa usitishaji vita kwa muda wa miezi miwili kufuatia pendekezo la Umoja wa Mataifa.
Hussein al Ezzi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, mzingiro dhidi ya wananchi wa Yemen ni jinai ya kivita na dhidi ya binadamu na unazuia kuongezwa muda wa usitishaji vita nchini humo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen ameongeza kuwa, ni aibu kwamba jukumu la nchi za Magharibi na Umoja wa Mataifa ni kutekeleza tu vikwazo na kuvihalalisha kuwa silaha ya kijeshi na kwamba nchi hizo haziheshimu sheria. Amesema jambo kama hili linashuhudiwa kwa mara ya kwanza katika historia.
Jumamosi iliyopita Abdulaziz bin Habtur Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye mfungamano na harakati ya Ansarullah alisisitiza kuwa, kurefushwa muda wa usitishaji vita kwa ajili ya masuala ya kibinadamu kunapasa kuzingatia hali ya kiuchumi na kifedha, haswa kutatua suala la ulipaji mishahara ya wafanyakazi, ambayo imesimamishwa tangu kuhamishiwa Benki Kuu katika mji wa Aden mwaka 2016.