Madai na tuhuma za Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah ya Lebanon zinaendelea kutolewa katika hali ambayo, makundi ya kisiasa ya Lebanon yanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu (2022).
Hujuma na tuhuma za utawala wa kifamilia wa Aal Saud dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon zinapigiwa upatu na watu wawili. Majuma mawili yaliyopita, Salman bin Abdul Aziz mfalme wa Saudia aliitaja Hizbullah kuwa ni harakati ya kigaidi ambayo kwa kufuata muamala wa kijeshi katika eneo la Asia Magharibi imekuwa ikitishia usalama wa taifa wa Kiarabu.
Juzi Walid Bukhari, balozi wa Saudia mjini Beirut Lebanon alikariri tuhuma za Mfalme Salman bin Abdul Aziz dhidi ya Hizbullah na kudai kwamba, harakati za chama cha Hizbullah ni za kigaidi na kwamba, kufanya kwake mambo kijeshi ni tishio kwa usalama wa taifa wa Kiarabu. Katika kuendelea na bwabwaja zake, balozi Bukhari alisema kuwa, harakati za kisiasa, kijeshi, kiusalama na kihabari za Hizbullah zinakwamisha mamlaka ya kujitawala ya Saudia pamoja na mataifa ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi.
Mbali na Wasaudi, ndani ya Lebanon pia kuna vibaraka wa Saudia ambao wanafanya mambo kwa mujibu wa matakwa ya utawala wa Riyadh ambapo wamekuwa wakitoa tuhuma dhidi ya Hizbullah.
Kimsingi ni kuwa, vibaraka hao ndani ya Lebanon wamekuwa wakitekeleza kwa niaba siasa za utawala wa Aal Saud kwa kuzihamasisha fikra za waliowengi na anga ya nchi hiyo iwe dhidi ya harakati ya Hizbullah.
Katika uwanja huo, Saad al-Hariri, Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon ametoa matamshi dhidi ya Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah akidai kwamba, Nasrullah ana uadui na Saudia. Saad al-Hariri amemhutubu Nasrullah akisema kwamba: Kung’ang’ania kwako kufanya uadui na Saudi Arabia na viongozi wa nchi hiyo, ni pigo la kuendelea dhidi ya Lebanon, nafasi yake na maslahi wa watu wa nchi hii.
Saad al-Hariri anatoa matamshi hayo katika hali ambayo mwaka 2017 alilazimishwa kubakia katika ardhi ya Saudia ambapo sambamba na utawala wa Riyadh kumlazimisha ajiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu, ulimzuia kutoka nchini humo na kurejea Lebanon.
Madai na tuhuma za ndani na za nje dhidi ya Hizbullah ya Lebanon zina sababu mbili kuu. Sababu ya kwanza ni kukinzana utambulisho wa Hizbullah na Saudia pamoja na washirika wake ndani ya Lebanon.
Hizbullah ni moja ya wachezaji wakuu na wenye taathira muhimu kwa mhimili wa muqawama ambao umekuwa na mchangao mkubwa katika matunda ya muongo mmoja uliopita ambapo mlingano wa nguvu umebadilika na kuwa kwa maslahi ya muqawama. Saudi Arabia inaona kuwa, nafasi na mafanikio haya ya Hizbullah yanakinzana na maslahi yake na ndio maana inafanya njama dhidi ya harakati hiyo.
Sababu nyingine inahusiana na uchaguzi wa Bunge wa Lebanon ambao umepangwa kufanyika Mei mwaka huu. Uchaguzi huu una umuhimu mkubwa katika medani ya kisiasa ya nchi hiyo. Hii ni kutokana na kuwa, Bunge lijalo la Lebanon linapaswa kumchagua Rais na Waziri Mkuu mpya.
Propaganda kubwa za utawala wa Aal Saud dhidi ya Hizbullah ya Lebanon zinafanyika kwa malengo ya kiuchaguzi ambapo Riyadh inafanya njama kuhakikisha kwamba, kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2018 muungano wa muqawama haupati ushindi.
Waitifaki na washirika wa Saudi Arabia ndani ya Lebanon akiwemo Saad al-Hariri pia ambaye huko nyumba amewahi kukwama kuunda Baraza la Mawaziri, wameelekeza nguvu na matumaini yao kwa uchaguzi ujao wa Bunge na kadiri idadi ya Wabunge wa Muungano wa Muqawama itakavyokuwa ndogo, ndivyo uwezekano wa wao kuwa na nafasi ya kuteua Waziri Mkuu utakavyokuwa mkubwa.
Katika uwanja huo, Ali Awadh Asseri balozi wa zamani wa Saudia nchini Lebaon alidai hivi karibuni kwamba, eti harakati za Hizbullah zinaipeleka Lebanon upande wa vita vya ndani suala ambalo si kwa maslahi ya nchi hiyo. Mwanadiplomasia huyo wa Saudia kwa kudai kwamba, Lebanon yote iko hatarini amesema bayana kwamba, kwa mtazamno wa kisiasa hegomonia na mamlaka ya Hizbullah yanapaswa kusambaratishwa. Hivyo wananchi wa Lebanon wanapaswa kuanzisha vuguvugu na kwenda katika masanduku ya kupigia kura.