Jumuiya na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yameelezea wasiwasi mkubwa yaliyonao kutokana na kuongezeka mno hatua za utawala wa Saudi Arabia za kuwanyonga kiholela wapinzani.
Jumuiya hizo zimewatolea mwito viongozi wa Saudia na mamlaka husika katika nchi hiyo ya utawala wa kifalme zikomeshe mauaji na hukumu za kiholela za adhabu ya kifo.
Mwito huo unatolewa huku kukiwa na uwezekano wa kutokea wimbi jipya la kunyongwa wafungwa na wanaharakati wa kisiasa na kijamiii walioko katika magereza ya Saudia baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Saudia lenye makao yake huko Ulaya limesisitiza kuwa, watawala wa Saudia wanapaswa kuheshimu haki za binadamu na kukomesha vitendo vya kuwanyonga kiholela watu.
Taasisi hiyo ilifichua hivi karibuni kuwa, hivi sasa watu wengine 15 wanasubiri kunyongwa na kuifanya idadi ya Wasaudia wanaosubiri kunyongwa kwa umati kufikia 53.
Wasiwasi wa duru na asasi za kimataifa kuhusu uwezekano wa kutendwa jinai nyingine na ukoo wa Aal Saud unatokana na ukweli kwamba utawala huo wa kiimla una rekodi iliyojaa jinai za mauaji ya halaiki na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mwezi Machi mwaka jana, utawala wa Aal Saud uliwanyonga kwa umati watu 81 kwa siku moja tu tena baadhi yao wakiwa ni raia wa nchi nyingine kama Yemen. 41 kati ya watu hao 81 walionyongwa kwa halaiki na ukoo wa Aal Saud walikuwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.