Saudia yakosolewa kwa kuzima sauti ya adhana kwa ajili ya hafla za ufuska

Licha ya ukandamizaji wa kimfumo wa utawala wa Saudia dhidi ya wale wanaokosoa mwelekeo wa kisiasa na kijamii wa utawala huo unaolazimishwa kwa watu kwa mabavu, sauti zimeanza kupazwa nchini humo dhidi ya hafla na sherehe za ufuska na ufisadi zinazoandaliwa na kile kinachoitwa Mamlaka Kuu ya Burudani katika Ufalme huo.

Makumi ya watu wameonekana kwenye video wakikosoa sera ya mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman na kusema kwamba, analenga kuwatumbukiza vijana kwenye ufuska kupitia mahfali na sherehe hizo zinazokiuka maadili.

Wanaharakati wa Saudia wamesambaza video nyingi katika mitandao ya kijamii wakisema zinaakisi hali ya ufisadi wa kimaadili unaoenezwa na Bin Salman katika jamii ya Saudia. Wananchi hao pia wamewataka viongozi wa Saudia kumwogopa Mwenyezi Mungu, kuheshimu mila na desturi za jamii, na kukomesha mahfali hayo ya kifuska, angalau kwa heshima ya maeneo matakatifu yanayotukuzwa na Waislamu wote duniani, yaani Makka na Madina.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Saudia vimesema kuwa, Bin Salman na Turki bin Abdul Mohsen bin Abdul Latif Al-Sheikh, mshauri katika Idara ya Ufalme mwenye cheo cha waziri na Mwenyekiti wa sasa wa Mamlaka Kuu ya Burudani, wanaelekea kupiga marufuku sauti za adhana za Swala misikitini kwa kipaza sauti kwa kisingizio kwamba wito huo wa Waislamu kwa ajili ya ibada unawakera watalii wanaokwenda kuhudhuria mahafali za densi nchini Saudia.

Baadhi ya wanaharakati wa mitandao ya kijamii wanahoji: Kwa nini Bin Salman anataka kuzuia adhana kwenye minara ya misikiti, wakati watu katika miji mingi ya Saudi hawalali tena kwa sababu ya sherehe kubwa za miziki zinazoendelea hadi usiku mkubwa?

Baadhi ya Wasaudi pia wanazungumza kwa huzuni baada ya mamlaka ya nchi hiyo kufanya maonyesho ya mitindo ya mavazi ya wanenguaji kadhaa wa kike katika mji mtakatifu wa Madina

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *