Saudi Arabia imemfunga jela miaka 15 daktari mmoja wa kike raia wa Tunisia kwa kuweka video ya maandamano ya kuiunga mkono Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon huko Tunisia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mahakama moja nchini Saudia imemuhukumu kifungo cha miaka 15 jela Bi Mahdiyah al Barzouqi kwa madai ya kuuvunjia heshima utawala wa kiukoo wa Saudi Arabia. Kosa pekee lililofanywa na daktari huyo raia wa Tunisia ni kuweka kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, video ya maandamano ya wananchi wa Tunisia waliokuwa wanaunga mkono Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Televisheni ya al Mayadeeni imemnukuu kaka wa daktari huyo akisema kuwa, dada yake mwenye umri wa miaka 51, amekuwa akiishi nchini Saudia tangu mwaka 2008 kwa ajili ya kufanya kazi ya udaktari. Askari usalama wa ukoo wa Aal Saud walimkamata mwaka 2020 kwa kuweka kwenye ukurasa wake wa Twitter, maandamano ya wananchi wa Tunisia ya kuiunga mkono Hizbullah ya Lebanon.
Daktari huyo amemtaka Rais Kais Said wa Tunisia na wanadiplomasia wa nchi yake wawashinikize viongozi wa Saudia wamuachilie huru. Lakini ikumbukwe hapa kwamba Rais Kais Said wa Tunisia ni katika waungaji mkono wa Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia.
Kwa miaka kadhaa sasa viongozi wa Saudi Arabia wamekuwa wakikandamiza watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuelezea mitazamo na maoni yao na wamekuwa wakitoa adhabu kali kwa kila anayeandika kitu ambacho hakikubaliani na msimamo wa utawala wa kiukoo wa Aal Saud.