Saudia yamhukumu kifo kijana kwa ‘kosa’ la kumuandalia futari mpinzani wa Ufalme

Shirika moja la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema mahakama ya Saudia imetoa hukumu ya kifo kwa kijana mmoja kwa ‘kosa’ la kumuandalia futari mpinzani wa ufalme katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Shirika la Umoja wa Ulaya la Haki za Kibinadamu la Saudia (ESOHR), katika ujumbe lililoweka kwenye ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumapili, lilimtaja kijana huyo kuwa ni Ahmed Al Daghaam. Alitayarisha futari hiyo katika siku ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu na kumpa mpinzani huyo wa utawala wa kidikteta wa Saudi Arabia ambaye anasakwa na jeshi la ufalme huo.

Ripoti hiyo inakuja wakati wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kwamba Ufalme wa Saudia unapanga kuwanyonga vijana wanane kutoka eneo la Qatif lenye wakazi wengi Waislamu wa madhehebu Shia katika Mkoa wa Mashariki.

Hayo yanajiri wakati ambao Wanaharakati wameanzisha kampeni chini ya alama ya kaulimbiu ya “Sitisha Uchinjaji” ya kutaka kufutwa kwa adhabu za kifo zinazotolewa kwa watoto wadogo na vijana.

Wamewataja mabarobaro hao wanaotarajiwa kunyongwa kuwa ni Abdullah al-Howaiti, Abdullah al-Derazi, Ali al-Sabiti, Hasan Zaki al-Faraj, Jalal Al Labad, Mahdi al-Mohsen, Javad Qariris na Yousef al-Manasif.

Wanaharakati hao wamesema kwamba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia imemhukumu Manasif na angalau wengine watano, akiwemo kijana anayeitwa Sajjad Aal Yassin, kifo kwa tuhuma bandia za kuacha imani yao ya Kiislamu.

Wameendelea kubainisha kuwa mabarobaro hao sita wako chini ya kesi katika Mahakama Maalumu ya Jinai ya Saudi Arabia (SCC) tangu Septemba 2019.

Hayo yanajiri huku ufalme wa kikoo Saudia unaoongozwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman ukishadidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani wanaotetea haki za kisiasa na kidini. Bin Salman kimsingi ndiye mtawala mkuu wa Saudia hivi sasa kutokana na hali mbaya ya kiafya ya baba yaje, Mfalme Mohammad bin Salman.

Jimbo la Mashariki limekuwa uwanja wa maandamano ya amani tangu Februari 2011. Waandamanaji wamekuwa wakiitisha mageuzi, uhuru wa kujieleza, kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, na kukomeshwa kwa ubaguzi wa kiuchumi na kimadhehebu dhidi ya eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Maandamano hayo yamekabiliwa na msako mkali wa utawala. Vikosi vya usalama vimeshadidisha ukandamizaji na ukatili katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *