Saudia yasema inajaribu kufanya mazungumzo na Iran ili kupunguza taharuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud anasema ufalme huo unajaribu kutafuta njia ya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama njia bora ya kutatua tofauti, huku kukiwa na mchakato wa kidiplomasia kati ya majirani hao wawili unaolenga kurekebisha uhusiano uliodorora.

Akizungumza katika jopo katika Jukwaa la Uchumi la Dunia huko Davos siku ya Jumanne, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Saudia alisema kuwa uamuzi wa nchi yake na mataifa mengine ya Ghuba ya Uajemi wa kuzingatia uchumi na maendeleo yao ni ishara kuwa badala ya mabishano ya jadi kuna uwezekano wa “kuelekea ustawi wa pamoja.”

Ameongeza, “Nadhani kadiri tunavyoweza kujenga hali ya ushirikiano katika kanda, ndivyo tunavyoweza kufanya kazi pamoja, ndivyo tunavyoweza kutoa sio tu ustawi kwa watu wetu, lakini pia kwa ukanda wetu wa karibu na kwingineko.”

Matamshi hayo yamekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian kuelezea matumaini yake siku ya Ijumaa katika ziara yake nchini Lebanon kwamba uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tehran na Riyadh unaweza kurejeshwa kupitia mazungumzo kati yao.

“Tuko tayari kurejesha uhusiano, na hatua kama hiyo itakuwa na athari chanya katika eneo zima,” Amir-Abdollahian aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Beirut.

Pia amesema hatua za kwanza zinapaswa kuwa kuanzishwa tena mazungumzo ya kufungua tena ubalozi mdogo wa Iran katika mji wa bandari wa Bahari Nyekundu wa Jeddah, na ubalozi mdogo wa Saudi Arabia katika mji mtakatifu wa kaskazini mashariki mwa Iran wa Mashhad kwa ajili ya raia wanaofanya safiri za kidini.

Amir-Abdollahian amewaambia waandishi wa habari kwamba, “kama tunavyoona, Saudi Arabia haiko tayari kabisa kuchukua hatua za kurekebisha mahusiano,”

Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na kunyongwa kwa kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudia, kuvamia ubalozi wake mjini Tehran.

Baadaye nchi hiyo ya kifalme ilitekeleza siasa za makabiliano dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hususan wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye watawala wa Saudia walikuwa na uhusiano wa karibu naye.

Saudi Arabia inaonekana hivi karibuni imebadilisha mkondo wake wa chuki, ikionyesha nia kupitia njia za kidiplomasia na pande tatu kurekebisha uhusiano na Iran na kurejesha uhusiano wa pande mbili.

Majirani hao wawili wamesalia kuwa na mgawanyiko mkubwa juu ya masuala kadhaa ya kikanda, hasa vita haribifu na vya muda mrefu vya Saudia dhidi ya Yemen.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *