Serikali ya Ethiopia: Jeshi linadhibiti asilimia 70 ya eneo linalotaka kujitenga la Tigray

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, asilimia 70 ya eneo linalotaka kujitenga la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo linadhibitiwa na vikosi vya jeshi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP, Rizwan Hossein, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ametangaza leo katika ujumbe wa Twitter: “70% ya Tigray iko chini ya udhibiti wa vikosi vya Wizara ya Ulinzi ya Taifa ya Ethiopia”.
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza pia kutumwa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na dawa na chakula, katika eneo hilo.
Hayo yanajiri, wakati siku ya Jumatano, vyanzo vya habari vilitangaza kuwa baada ya miaka miwili ya mzozo kati ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, pande hizo mbili zimetia saini makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji mkuu wa Afrika Kusini.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alisema kuhusiana na hilo: “mkataba wa amani tuliosaini na harakati ya Tigray ni muhimu sana kwa Ethiopia kuelekea kwenye ufanyaji mageuzi”.

Mazungumzo kati ya jeshi la Ethiopia na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, yalianza tarehe 25 Oktoba huko Pretoria, mji mkuu wa Afrika Kusini. Mnamo tarehe 5 Oktoba, pande hizo mbili ziliukubali wito wa Umoja wa Afrika wa kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu.
Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia limekuwa likishuhudia mzozo na mapigano kati ya wanamgambo wa kundi la TPLF na jeshi la nchi hiyo tangu Novemba 2020. Idadi kubwa ya raia wameuawa na wengine takribani milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *