Serikali ya India imebomoa msikiti mwingine katika jimbo la Uttar Pradesh kwa kisingizio cha ujenzi wa barabara.
Viongozi wa India wangali wanaendeleza sera zao za kibaguzi dhidi ya Waislamu, na mara hii sera hiyo imeonyeshwa kwenye video ya kubomolewa msikiti katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ukurubishaji Madhehebu za Kiislamu, vyombo vya habari na duru za India zimeripoti kuwa msikiti wa Shaahafi ulioko katika jimbo la Uttar Pradesh umebomolewa kwa kisingizio cha ujenzi wa barabara.
Video hiyo iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, inaonyesha msikiti huo ukibomolewa katika tukio lililoshuhudiwa na watu kadhaa.
Katika video hiyo, linaonekana kwanza buldoza likiubomoa msikiti huku malori yakisubiri kuondoa kifusi kilichokusanywa kufuatia kubomolewa msikiti huo.
Kabla ya hapo, kamera zilirekodi hujuma iliyofanywa na makumi ya Wahindu wenye itikadi kali ya kuuvamia msikiti katika jimbo la Hyderabad wakati Waislamu wakiwa wanasali.
Waliosambaza filamu hiyo wameeleza kuwa, mbali na Wahindu hao wenye msimamo mkali kuwashambulia Waislamu, waliingiza kwa nguvu pia masanamu yao msikitini humo.
Itakumbukwa kuwa mnamo Desemba 1992 msikiti maarufu wa Babri ulibomolewa katika hujuma iliyofanywa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka wakiungwa mkono na chama tawala nchini India, ambapo zaidi ya Waislamu elfu mbili pia waliuawa.
Kukabidhi ardhi ya Msikiti wa Babri kwa Wahindu, kufuta mamlaka maalum liliyopewa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India ya kujiendeshea mambo yake, kufuta uraia wa mamia ya maelfu ya Waislamu na kupitisha sheria mpya ya uraia ya kutoa uraia kwa wasio Wahindi kwa masharti kwamba wasiwe Waislamu, ni baadhi tu ya maamuzi yaliyopitishwa na serikali ya India dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Kuna takriban Waislamu wapatao milioni 250 kati ya raia zaidi ya bilioni moja na milioni 400 wa India..