Serikali Ya Kenya Yatoa Sh34 Bilioni Za Kukabiliana Na Kero Ya Uhaba Wa Mafuta

SERIKALI imetenga Sh34,446,813,295 katika bajeti ya ziada ya mwaka huu katika mpango wa kupunguza bei ya mafuta ili kukinga Wakenya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu, Aprili 5, 2022, kutia saini Mswada wa Bajeti ya Ziada uliopitishwa bungeni wiki jana.

Hatua hiyo itatoa afueni kwa waendeshaji magari na wahudumu wa bodaboda nchini ambao wamekuwa wakihangaika tangu wiki jana kutokana na uhaba wa mafuta katika miji mbalimbali nchini.

Duru katika sekta ya mafuta inasema kuwa hali hiyo imechangiwa na hatua ya kampuni za kuuza mafuta nchini kuhodhi bidhaa hizo kama hatua ya kuishinikiza serikali iwalipe malimbikizi ya pesa za kufidia hasara wanazopata kwa kuuza bidhaa hiyo kwa bei iliyowekwa na serikali.

Tangu bei ya mafuta ilipoanza kupanda katika masoko ya kimataifa mwezi Septemba mwaka 2021 serikali haijaongeza bei ya bidhaa hiyo kwa kiwango sawa. Badala yake ilianzisha mpango wa kuzilipa kampuni za kuuza mafuta nchini fedha za kufidia hasara ambayo wangepata.

Kwa mfano, japo mwezi jana – Machi – serikali iliongeza bei ya mafuta aina ya petroli kwa Sh5, kutoka Sh129 hadi Sh134 kwa lita moja jijini Nairobi, bei hiyo ingefika Sh150 kwa lita endapo serikali haingeanzisha mpango wa kuziruzuku kampuni za mafuta.

Kupanda kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa kumechangiwa na ongezeko la hitaji ya bidhaa hiyo kufuatia ongezeko la shughuli katika mataifa ya ulimwengu baada ya kupunguza kwa msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

Kwa mfano mnamo Februari, 2022 bei ya mafuta aina ya petroli ilipanda kwa kima cha asilimia 13.4 hadi dola za Amerika 676 (Sh77,109) kwa pipa ikilinganishwa na dola 596 (Sh68,035) mwezi wa Januari 2022.

Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Urusi kuvamia Ukraine mnamo Februari 24, 2022 hatua ambayo ilichangia mataifa ya Magharibi kuiwekea Urusi vikwazo.

Vikwazo hivyo, vilivuruga uwezo wa Urusi kuuza mafuta yake katika mataifa mengi ya nje ikizingatiwa kuwa taifa hilo ndilo la pili katika uzalishaji mafuta kwa wingi duniani.

Biashara nyingi nchini Kenya zimeathiriwa na kero ya ukosefu wa mafuta. Lakini kinaya ni kwamba serikali, kupitia Kampuni ya Usambazaji Mafuta Nchini (KPC) imeshikilia kuwa kuna mafuta ya kutosha nchini.

Hatua ya Rais Kenyatta kutia saini Mswada huo Ziada wa Bajeti pia itawezesha kutolewa kwa Sh139,752,936,287 kutoka Hazina ya Kitaifa kufadhili mpango wa kushughulikia makali ya ukame, operesheni za kiusalama, maandilizi ya uchaguzi, ulipaji wa malimbikizo ya madeni ya asasi za umma, miongoni mwa mahitaji mengine ya dharura.

Kwa mfano, sekta ya usalama imetengewa Sh950 milioni zaidi za kuwaajiri maafisa wapya wa polisi ili kuimarisha usalama nchini, kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Nayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetengewa Sh 8,813, 903, 557 zaidi kuiwezesha kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wizara ya Ulinzi nayo imetengewa Sh1.4 bilioni zaidi kuiwezesha Shirika la Nyama Nchini (KMC) kuendesha mpango wa kununua mifugo iliyodhoofishwa na ukame.

Wizara ya Ugatuzi pia imetengewa Sh1.2 bilioni zaidi kufadhili mipango mingine ya kuzuia makali ya ukame na baa la njaa ambayo inaathiri jumla ya kaunti 23.

Idara ya Huduma za Kijamii, Masilahi ya Wakongwe na Mipaka Maalum imetengewa Sh2.4 bilioni zaidi kufadhili mpango wa ununuzi wa chakula cha msaada kuzifaa familia zilizoathiriwa na makali ya ukame.

Tume ya Huduma za Walimu (TSC) nayo imetenngewa Sh6.9 bilioni kugharamia mishahara walimu wanaotoa mafunzo chini ya mtaala wa umilisi na utendaji (CBC).

Wizara ya Elimu nayo imetengewa Sh2 bilioni zaidi katika Bajeti hiyo ya Ziada za kudhili ujenzi wa madarasa zaidi ya kuwezesha mpito kutoka mfumo wa 8.4.4 hadi mfumo mpya wa.

Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) nayo imetengewa Sh4.9 bilioni kuhakikikisha kuwa miradi mbalimbali iliyoanzishwa imekamilishwa. Pesa hizo pia zitatumia kugharamia basari za wanafunzi shule zikitarajiwa kufunguliwa mnamo Aprili 27, 2022 kuashiria kuanza kwa mwaka wa masomo wa 2022.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *