Serikali ya Senegal imepunguza ufikiaji wa huduma za intaneti na simu za mkononi katika baadhi ya maeneo kwa sababu ya ghasia mbaya ambapo jumbe za “chuki na uasi” zimetumwa mtandaoni.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi imekumbwa na maandamano na ghasia kwa muda wa siku tatu ambapo ambapo watu 16 wameuawa. Ghasia hizo ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Wiki iliyopita, serikali ilizuia upatikanaji wa baadhi majukwaa ya mitandao, lakini watu wengi waliweza kujipenyeza katika mitandao iliyofungwa kwa kutumia mfumo wa VPN ambao huficha eneo la mtumiaji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Senegal, Antoine Félix Diome amesema serikali imebana mitandao ya kijamii, ili kuzuia usambazaji wa jumbe za chuki na za kichochezi wakati huu wa fujo.
Ghasia zilizuka kwa mara ya kwanza Alhamisi, baada Ousmane Sonko kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya “kuwafisidi vijana.”
Sonko, ambaye hakuhudhuria kesi yake mjini Dakar, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Wakili wake alisema hati ya kukamatwa kwake bado haijatolewa.
Sonko alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais wa Senegal 2019 na anapendwa na vijana wa nchi hiyo. Wafuasi wake wanaamini kuwa kifungo hicho ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha hagombei katika uchaguzi wa urais wa 2024.
Sonko anachukuliwa kuwa mshindano mkuu wa Rais Macky Sall na amemtaka Sall kutamka hadharani kwamba hatawania muhula wa tatu madarakani.
Taasisi muhimu za Kiafrika, yaani Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) tayari zimelaani ghasia zilizozuka Ijumaa nchini Senegal.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani “vikali” ghasia hizo na kusema, “Vitendo kama hivyo vinaharibu sifa ya demokrasia ya Senegal, ambayo Afrika imekuwa ikijivunia. Aidha amewataka wahusika wote kutulia na kushiriki katika mazungumzo.
Umoja wa Afrika pia umetoa wito kwa serikali ya Senegal kuheshimu haki ya maandamano ya amani.
ECOWAS imesikitishwa na kupotea kwa maisha ya watu na kutoa wito wa “kuzuiliwa na kusuluhisha mizozo kwa njia za amani.”
Kuzimwa intaneti ili kuzuia ghasia za wapinzani ni jambo la kawaida barani Afrika na lilianza mnamo 2011 wakati watawala wa Misri, Tunisia na Libya walipojaribu kudhibiti kuenea kwa habari wakati wa mwamko wa wananchi. Tangu wakati huo Gabon, Gambia, Uganda, Tanzania Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimewahi kuzima intaneti wakati wa uchaguzi au wakati kunapoibuka ghasia.