Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametangaza rasmi kuwa nchi hiyo imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa Ebola na amewapongeza raia wa Uganda kwa kuwa makini katika kupambana na ugonjwa huo.
Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni na redio, Rais Yoweri Museveni amsema: ‘’Hakuna tena Ebola nchini. Tumeishinda Ebola kwa sababu watu wamesikiliza.”
Aidha amewashukuru wafanyakazi wa matibabu kwa kufanya kazi bila kuchoka katika kupambana na mripuko huo. Ameahidi kuwatunuku nishani wafanyikazi bora wa matibabu ambao wamesaidia katika kupambana na ugonjwa huo.
Jumamosi wiki hii, Makamu wa Rais wa Uganda, Bi Jessica Alupo aliondoa rasmi marufuku ya Ebola katika wilaya za Kassanda na Mubende, ambazo ndizo zilizokuwa kitovu cha mripuko wa ugonjwa huo.
Bi Jessica Alupo amesema, “Ni siku 89 leo tangu mripuko wa ugonjwa wa Ebola utangazwe katika Wilaya ya Mubende na tumekuwa tukikabiliana na mripuko huu tangu wakazi huo. Pia ni siku 63 tangu wilaya za Mubende na Kassandra kuwekwa chini ya karantini na sheria kali za kukabiliana na Ebola.”
Vile vile alisema: “Kwa siku 34 sasa wilaya ya Mubende haijasajili kesi yoyote iliyothibitishwa ya Ebola na wilaya ya Kassanda nayo haijasajili mgonjwa hata mmoja wa Ebola kwa siku 37 sasa, ndio maana tumeamua kuondoa masharti na sheria kali za kukabiliana na ugonjwa huo.”
Akitangaza rasmi kudhibitiwa ugonjwa huo, Rais Museveni amesema jumla ya watu walioambukizwa Ebola ni 142, watu 86 wamepona na vifo 56 vimerekodiwa.
Uganda iimekuwa ikipambana kudhibiti ugonjwa wa Ebola unaoenea haraka tangu mripuko wa ugonjwa huo ulipotangazwa mwezi Septemba mwaka huu.