Serikali yaikabidhi NMB bustani ya Forodhani

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMS) imefikia makubaliano ya kuikabidhi benki ya NMB kutunza bustani ya Forodhani visiwani hapa ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuunga mkono uhifadhi wa mazingira na ajenda ya uchumi wa bluu.

Mradi huo wa utunzaji wa bustani ya Forodhani unalenga kuboresha mazingira ya kitalii na kuakisi vyema sifa maarufu ya eneo hilo, na utawezesha bustani hiyo kuvutia wageni wengi zaidi kila mwaka huku ukichangia kuchochea sekta ya utalii.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar wakati wa kutangaza Mashindano ya Mbio za Boti, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Magharibi, Rashid Simai Msaraka alisema benki hiyo imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo na kusaidia utekelezaji wa mipango ya Setikali.

Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk Hussein Mwinyi imeweka kipaumbele cha kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi na kuzitaka kampuni nyingi kuunga mkono mipango ya maendeleo ya serikali.

“Tumefanya kazi kwa karibu na benki hii katika miaka ya nyuma na nimedhihirisha na kutangaza kuwa tayari tumefikia makubaliano ya kuendeleza na kutunza bustani za Forodhani,” Msaraka alisema.

Alibainisha kuwa pamoja na kuboresha mandhari ya eneo hilo, mradi huo utaleta manufaa makubwa na kwamba, kazi hiyo itafanywa na wakandarasi wazawa.

“Tuna matumaini makubwa kuwa mbali na kutengeneza nafasi za kazi, mradi huu utasaidia kupendezesha na kuimarisha jiji letu kwa sababu eneo hilo ni mojawapo ya vivutio vikubwa hapa,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Kadi wa NMB, Phillbert Casmir wakati wa hafla hiyo alisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kusaidia ushirikishwaji wa fedha na kuongeza kuwa itaendelea kutoa bidhaa zinazokidhi matakwa ya wateja.

Alisema mipango ya benki hiyo ni kuendelea kupeleka huduma karibu na wateja huku akiongeza kuwa benki hiyo ina mpango wa kupeleka huduma kwenye maeneo ya Wete, Nungwi, Mkoani, Uwanja wa ndege miongoni mwa maeneo mengine visiwani humo.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *