Dar es Salaam. Dhamira ya Serikali kuongeza kasi ya ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya uzalishaji mali na kukuza uchumi, imeendelea kuungwa mkono na taasisi za fedha mbalimbali nchini.
Benki ya NMB ni sehemu ya mtekelezaji mkubwa wa mkakati huo wa Serikali ambapo, imeendelea kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini kwa kuwapa mikopo yenye masharti na gharama nafuu ili kuhakikisha wanapiga hatua kiuchumi.
Tayari benki hiyo imetoa mikopo ya zaidi ya Sh752.7 bilioni kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kipindi cha kati ya Julai 2021 hadi Juni 2022, ambapo mikopo 37,501 ilitolewa.
Afisa Mkuu Huduma Shirikishi wa NMB, Nenyuata Mejooli akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya NMB iliyofanyika kwenye banda la Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), leo Jumanne ya Julai 5, 2022 amewakumbusha wanawake wajasiriamali kubuni bidhaa zenye ubora.
Amesema benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kuanzia Sh500,000 hadi Sh75 milioni ukiwa ni mkakati mahususi wa uwezeshaji wanawake tangu mwaka 2000.
Amesema kutokana na dhamira ya benki yake, benki hiyo imeorodhesha hati iliyopewa jina la NMB Jasiri Bond katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ambayo ilikusanya Sh74.2 bilioni ikilenga biashara zinazomilikiwa na wanawake.
“Fedha zilizopatikana zitatumika kusaidia biashara zinazomilikiwa na wanawake au wafanyabiashara ambao mnyororo wao wa thamani unanufaisha wanawake wengi. Natoa wito kwa wanawake wajasiriamali kuchangamkia fursa tunapoanza kutoa mikopo,” amesema.
Ameongeza kuwa benki yake tayari imetoa Sh95.1 bilioni katika miaka mitatu iliyopita kama sehemu ya juhudi zake za kusaidia ukuaji wa biashara zinazomilikiwa na wanawake nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla amesema hatua ya benki hiyo kusaidia kuwawezesha wanawake inapaswa kuunga mkono.
“Kuna fursa zimewekwa kwa wanawake katika mchakato wa zabuni na manunuzi, lakini kwa bahati mbaya hawajaweza kushiriki kikamilifu na kunyakua fursa kama hizo.
Wanawake wanahitaji kutumia fursa hizi zote kikamilifu. Kama chama, tutaendelea kuhamasisha wanawake kuhusu jinsi ya kunyakua fursa kama hizo kuanzia ngazi ya chini,” amesema.
Maadhimisho ya Siku ya NMB yalifanyika chini ya kaulimbiu ya “Kuwawezesha Wanawake katika Biashara” yamewakutanisha wanawake kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Simiyu, Tanga, Mara, Njombe, Mwanza kutoka sekta ya usindikaji wa vyakula, nguo, ngozi, vipodozi, afya na kazi za mikono.