Shaka aipongeza MNH kufanikisha upasuaji pacha walioungana

Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kufanikisha upasuaji wa kutenganisha watoto Neema na Rehema walioungana na kuwaweka katika uangalizi mzuri.

Upasuaji huo uliodumu kwa kwa saa saba, ulifanikiwa licha ya changamoto kubwa kwa watoto hao kuungana ini, moyo na baadhi ya tishu za ndani na ulitekelezwa na wataalamu wa afya 31 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bahrain na Ireland wanaotokea shirika la Operation Child Life.

Akizungumza leo Julai 2, 2022 akiwa hospitalini hapo, Shaka amempongeza Amina Amos (18) ambae ni mama mwenye watoto waliofanyiwa upasuaji.

“Ni jambo la kujivunia kwa kuwa upasuaji huu ambao umefanyika kwa Afrika Mashariki na Tanzania ndio wa kwanza na kwa Afrika ni nchi ya tatu,” amesema Shaka.

Amesema upasuaji huo uliofanyika jana unaonesha ni namna gani uwekezaji uliofanywa katika Sekta ya afya unavyoanza kuzaa matunda.

“Kwa hili ningependa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya,” amesema Shaka.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *