Shambulio la kigaidi katika Haram ya Shah Cheragh; mfano mwingine wa mradi wa kuvuruga usalama wa Iran

Ikiwa ni katika kuendeleza mradi wa maadui wa kuvuruga usalama na kuibua machafuko nchini Iran, siku ya Jumatano idadi kubwa ya wafanyaziara katika Haram takatifu ya Ahmad bin Musa (as) huko katika mji wa Shiraz waliuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi lililotekelezwa katika haram hiyo.

Jumatano alasiri gaidi mmoja wa kundi la matakfiri aliingia kwenye Haram ya Ahmad bin Musa (Shah Cheragh) katika mji wa Shiraz na kuwashambulia kwa risasi za bunduki waumini waliokuwa wakitekeleza ibada katika eneo hilo takatifu. Watu 15 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika tukio hilo la kigaidi, akiwemo mwanamke mmoja na watoto wawili wadogo. Kundi la kigaidi na matakfiri wa Daesh limetangaza kuhusika na jinai hiyo.

Shambulio hilo la kigaidi limetekelezwa katika hali ambayo katika wiki za hivi karibuni maadau wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametumia nguvu zao zote za kisiasa na vyombo vya habari kwa lengo la kuchochea ghasia na machafuko hapa nchini. Kwa mujibu wa Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, shambulio hilo la kigaidi limeweka wazi nia na malengo maovu yanayofuatiliwa na wachochezi wa machafuko na ugaidi katika ardhi ya Iran. Amesisitiza kwamba kuna habari za kuaminika na za kutosha zinazothibitisha kwamba maadui wanatekeleza mradi mkubwa wa kuvuruga usalama na uthabiti wa Iran.

Uzoefu wa miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unathibitisha wazi kuwa maadui daima wanatumia mbinu tofauti zikiwemo za ugaidi, kuchochea machafuko na ghasia na kutumia mashinikizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi kwa shabaha ya kuzuia kufikiwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na kufikiwa maendeleo na kuimarisha umoja na mshikamano nchini.

Tangua siku za mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusambaratika siasa za madola ya kiistikbari duniani, Iran imekuwa ikitazamwa kwa jicho la chuki na hasira na mataifa hayo ya Magharibi pamoja na vibaraka wao yakiwemo makundi ya Muanafiqeen na Matakfiri. Kufikia sasa zaidi ya Wairani 17,000 wakiwemo wasomi na viongozi wa ngazi za juu serikalini wamepoteza maisha yao katika vitendo vya ugaidi unaochochewa na maadui wa serikali ya Kiislamu nchini.

Maadui wa Iran wakiongozwa na Merekani na utawala wa kigaidi wa Israel, katika miaka ya karibuni wamekuwa wakiwaunga mkono magaidi kwa njia mbalimbali ndani ya ardhi ya Iran na katika eneo, kwa lengo la kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kutoa mafunzo ya kijeshi na kigaidi, silaha, kusafirishwa chakula na silaja za aina tofauti kwa makundi ya kigaidi pamoja na kuwapa zana na vifaa mbalimbali vya mawasiliano kupitia ndege za mizigo zinazopaa katika maeneo yanayodhibitiwa na magaidi wa Daesh ni sehemu ndogo tu ya misaada na uungaji mkono unaotolewa na Marekani na washirika wake kwa magaidi hao ili kuidhuru Iran kwa njia moja au nyingine. Magaidi hao wanaohudumia maslahi ya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel wametekeleza ugaidi wa kutisha katika ardhi ya Iran ikiwa ni pamoja na kuwaua wanasayansi, walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na raia wa kawaida wasio na hatia yoyote kama tulivyoona juzi katika Haram ya Shah Cheragh huko Shiraz.

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanadhani kwamba kupitia vitendo hivyo vya ugaidi wanaweza kuizuia Iran kufikia malengo yake ya Mapinduzi ya Kiislamu huku wakiwa wameghafilika na ukweli kwamba taifa la Iran daima limekuwa likidumisha malengo na njia ya mashahidi na bila shaka damu ya mashahidi imawasaidia pakubwa katika kuendeleza njia hiyo tukufu inayoidhaminia Iran malengo yake matukufu.

Ni wazi kwamba jinai iliyotekelezwa hivi karibuni na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku nchi zinazodai kutetea haki na kupambana na ugaidi zikiwa zimenyamaza kimya, kwa mara nyigine tena imeanika wazi unyama na uovu wa nchi hizo na vibaraka wao. Kama alivyosema Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maadui wameamua kutumia ugaidi dhidi ya taifa la Iran ili kulipiza kisasi cha pigo kubwa walilopata na kushindwa kufikia malengo yao maovu nchini, lakini pamoja na hayo watambue kwamba vyombo vya usalama na polisi nchini watawafuatilia kwa makini wahusika wa jinai ya hivi karibuni na kuwaadhibu vikali wapangaji na watekelezaji wote wa jinai hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *