Maelfu kadhaa ya polisi na vikosi vya usalama vya Shirikisho la Ujerumani vilivamia na kushambulia makao kadhaa ya kundi la mrengo wa kulia katika operesheni iliyofanyika katika pembe tofauti za nchi hiyo Jumatano asubuhi.
Inasemekana kwamba wanachama wa kundi hilo walikuwa wamepanga kushambulia bunge la Ujerumani siku ambayo haikutajwa na kupindua serikali kwa kutumia nguvu. Mwendesha Mashtaka wa Shirikisho la Ujerumani ametangaza kushiriki kwa takriban polisi elfu tatu katika maeneo 130 katika majimbo 11 ya nchi hiyo dhidi ya kundi hilo la mrengo wa kulia linalojulikana kama “Reich Citizens.”
Wanachama wa kundi hilo ambao baadhi ni wanajeshi wa Ujerumani hawaamini katiba wala mipaka ya Ujerumani ya baada ya Vita vya Pili vya Dunia na wanataka kupinduliwa serikali ya Berlin.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Shirikisho la Ujerumani inasema kwamba operesheni hiyo iliyofanyika Desemba 7, iliwakamata raia 22 wa nchi hiyo kwa tuhuma za kuwa wanachama wa kundi hilo la “kigaidi”.
Raia 3 wa kigeni akiwemo Mrussia pia wamekamatwa kwa tuhuma za kuunga mkono kundi hilo la kigaidi.
Ujerumani, ikiwa ni nchi muhimu zaidi ya Umoja wa Ulaya na uchumi mkubwa zaidi barani humo, na hata kabla ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, imekuwa kituo muhimu cha shughuli za makundi ya mirengo ya kulia yenye misimamo na fikra za kupindukia mipaka, kutokana na sababu mbalimbali za kihistoria, kitamaduni na kijamii, suala ambalo lilipelekea kuingia madarakani kwa utawala wa Kinazi ulioongozwa Adolf Hitler. Fikra zake kali hatimaye ziliibua Vita vya Pili vya Dunia, ambavyo vilisababisha maafa makubwa ya mamilioni ya watu na kuharibiwa miundombinu mingi ya Ujerumani na kisha kugawanywa nchi hiyo katika sehemu mbili tofauti, yaani Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi.
Baada ya kuungana Ujerumani mbili, harakati na makundi ya Unazi mamboleo ambayo yana mielekeo mikali ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahamiaji yamekuwa yakitaka Ujerumani ibakie kuwa kile yanachokitaja kuwa ‘safi’, makundi ambayo yamekuwa yakiongezeka taratibu katika nchi hiyo ya Ulaya.
Fikra hizo za ubaguzi wa rangi ziliongezeka hasa baada ya mzozo wa wakimbizi barani Ulaya mwaka 2015 ambapo zaidi ya wakimbizi milioni moja walikimbilia nchini Ujerumani, na kupelekea kuibuliwa hisia kali za mrengo wa kulia na vyama vya kibaguzi kama vile vuguvugu la “Pegida” na chama cha “Alternative for Germany AfD.”
Katika uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge nchini Ujerumani, chama hicho chenye siasa kali za mrengo wa kulia kilipata ushindi mkubwa, jambo ambalo linaonyesha kuongezeka fikra na mielekeo ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahamiaji katika nchi hiyo ya Ulaya.
Viongzi wa Ujerumani wameelezea wasiwasi wao kuhusu nafasi ya chama cha Alternative for Germany katika kujenga mazingira ya chuki dhidi ya wahamiaji na serikali ya nchi hiyo.
Wakati huo huo, makundi ya Wanazi mamboleo pia yamepata uhai mpya katika miaka ya hivi karibuni ambapo yamekuwa yakitekeleza siasa za mabavu na ugaidi ili kufikia malengo yao.
Mfano wa wazi wa ukweli huo ni kundi la mrengo wa kulia lenye fikra za kuchupa mipaka linalojiita “Reich Citizens”, ambalo limepata ushawishi mkubwa na kuenea kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, kwa namna ambayo hata limejipenyeza katika safu za jeshi la Ujerumani.
Jarida la Spiegel liliandika katika muktadha huu kwamba kambi za kijeshi za kikosi maalumu cha Ujerumani katika mji wa Calau ulioko kusini-magharibi mwa Uherumani ni miongoni mwa maeneo ambayo operesheni ilifanyika siku ya Jumatano dhidi ya wafuasi wa kundi hilo la Wanazi mamboleo.
Kituo hicho cha kijeshi pia siku za nyuma kiliibua utata kutokana na tuhuma za uwezekano wa kupenya humo fikra na mielekeo ya mrengo wa kulia wenye kufurutu ada na kuathiri baadhi wa wanajeshi wa Ujerumani. Wasiwasi kuhusu kupenya fikra za Wanazi mamboleo katika jeshi la Ujerumani unarudi nyuma hadi 2017 ambapo nembo za kinazi zilipatikana katika kambi za kijeshi.
Mnamo Machi 2020, maafisa wa jeshi walitangaza kuwa walikuwa wamegundua watu 27 wenye itikadi kali za mrengo wa kulia katika jeshi la Ujerumani. Mwaka mmoja au miwili iliyopita, maafisa wa Ujerumani walionya kwamba takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa harakati zinazotia wasiwasi za watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia katika nchi hiyo.
Mnamo Mei 2021, Horst Seehofer, Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo wa Ujerumani, alisisitiza kwamba mrengo wa kulia wenye misimamo ya kupindukia mipaka ndio tishio kubwa zaidi kwa Ujerumani na kusema: Jinai zilizofanywa na mrengo huo mwaka uliopita ziliongezeka kwa asilimia 5.65, kiwango ambacho ni zaidi ya nusu ya jinai zilizoainishwa kama “zilizotekelezwa kwa nia za kisiasa.”
Kabla ya hapo, kundi jingine la Ujerumani kwa jila la “National Socialist Underground NSU” liligundulika kuhusika na jinai za mabavu zilizotekelezwa kati ya 1998 na 2011, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikabila ya wanaume tisa wahamiaji na afisa wa polisi kutokana na mielekeao ya ubaguzi wa rangi.
Inaonekana kwamba kutokana na kuzorota kwa hali ya kiuchumi na kijamii nchini Ujerumani, harakati za makundi ya Wanazi mamboleo ambayo yanachochea ubaguzi wa rangi na kutumia silaha, na hata kupindua serikali ili kufikia malengo yao yanayochupa mipaka, zitaongezeka na kuwa na nafasi na ushawishi mkubwa zaidi katika jamii ya Ujerumani katika siku zijazo.
Operesheni iliyotekelezwa siku ya Jumatano na polisi ya Ujerumani katika pembe tofauti za nchi hiyo ya Ulaya inathibitisha wazi kuongezeka kwa makundi ya Wanazi mamboleo kama vile “Reich Citizens” katika nchi hiyo.