Makundi ya wananchi ya kupambana na ugaidi nchini Iraq yametaka kuondolewa nchini humo mara moja vikosi vya kigeni yakisema kuwa hatua ya serikali ya eneo la Kurdistan ya kualika katika eneo vibaraka wa Mossad inawafanya Wairaki kuwa shabaha ya kulengwa na upande wowote unaopinga vibaraka hao.
Ikizungumza jana Jumapili kuhusu shambulio lililofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah dhidi ya kituoa cha shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel Mosad katika eneo la Erbil huko Kurdistan ya Iraq, harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya an-Nujaba imetahadharisha kwamba uwepo wa maajenti na vibaraka wa Mossad katika ardhi ya Iraq unazifanya pande zinazohasimiana na utawala wa kibaguzi wa Israel kulenga vituo vyao katika nchi hiyo. Imesema operesheni ya Erbil ililenga kituo cha mamluki wa Kizayuni ambao wanapewa hifadhi na familia moja mashuhuri katika mji huo, ikimaanisha familia ya Barzani, ambayo imekuwa ikitawala siasa za Kurdistan kwa miaka mingi.
Akram al-Kaabi, Katibu Mkuu wa harakati ya an-Nujaba amesema familia ya Barzani inatoa hifadhi kwa maadui wa Iraq kwa lengo la kudhoofisha nchi na kutenganisha Kurdistan na Iraq. Ameendelea kusema: “Tunawapongeza wale waliosimama na sisi dhidi ya Daesh na Mossad,” kidhahiri akimaanisha Iran ambayo ilikuwa na nafasi muhimu nchini Iraq katika kushinda na kuwafukuza magaidi hao wa kitakfiri katika miji tofauti ya nchi hiyo. Amesema harakati hiyo imethibitisha kwamba mamluki kadhaa wa Mossad waliuawa katika operesheni hiyo Sepah.
Kundi jingine la mapambano ya Kiislamu la Iraq kwa jina la Kata’ib Hezbullah nalo limesisitiza haja ya kufungwa na kuharibiwa kambi zote za kijeshi na kijasusi za kigeni katika ardhi ya nchi hiyo ili kuepusha mzigo zaidi wa migogoro ya kimataifa na kikanda kwenye ardhi ya nchi hiyo.