Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, mshindi halisi wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qatar ni taifa la Palestina kutokana na wimbi kubwa la wachezaji na mashabiki wa soka kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Sheikh Ali Da’mush amebainisha kuwa, matukio mbalimbali yanayoshuhudiwa hivi sasa katika mashindano ya Kombe la Dunia nchini Qatar yanaonyesha wazi kwamba, mshindi halisi wa mashindano hayo ni Palestina kwani kumekuwa na uungaji mkono mkubwa mno kwa taifa hilo.
Aidha ameeleza kuwa, Kombe la Dunia nchini Qatar limeonyesha pia kupingwa vikali mchezo mchafu wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Isarel na kwamba, Israel na washirika wake wamefeli katika mpango huo kwani wananchi wa mataifa mbalimbali hasa ya Kiarabu wamekuwa wakiingia viwanjani au kushangilia ushindi wa timu zao wakipeperusha bendera ya Palestina.
Kadhalika Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema: Palestina imebakia katika akili na nyoyo zenye dhamira safi za wananchi wa mataifa ya Kiarabu na katika ndimi za vijana wanaoshuhudia mechi mbalimbali za Kombe la Dunia nchini Qatar, huku Israel ikitengwa kikamilifu.
Moja ya matukio ya kuvutia katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar ni kukataa wananchi wa mataifa mbalimbali ya Kiarabu kuhojiwa na vyombo vya habari vya Israel na vilevile kuiunga mkono Palestina dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeashiria matatizo makubwa yanayowakumba waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea hivi sasa nchini Qatar na kuandika, katika mashindano haya tumeelewa ni kiasi gani hatupendwi na tunachukiwa vibaya katika ulimwengu wa Kiarabu.