Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama amesema kuwa, walioanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel wamejitia matatani.
Sheikh Maher Hammoud amesifu mchango na nafasi ya mashahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis katika kukabiliana na njama chafu za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kueleza kwamba, mataifa yaliyoamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel yamejiuza.
Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama amesema hayo katika hafla iliyofanyika kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut, Lebanon kwa mnasaba wa mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Lutenii Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha’abi na kubainisha kwamba, makamanda wa muqawama ni wawakilishi wa haki na njia ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha’abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi vamizi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Hujuma hiyo ilitekelezwa kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.