Sheikh Naim Qassim: Hujuma za kihabari na kigaidi za Marekani dhidi ya Iran zimegonga mwamba

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, hujuma za kihabari na kigaidi za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilizokuwa zikiendeshwa katika fremu ya machafuko yaliyokuwa yameibuka nchini Iran zimesambaratika na kugonga mwamba.

Samahat Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, njama chafu za Marekani zilizoendeshwa katika kipindi cha kuibuka machafuko kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amin zimefeli na kwamba, Iran inaendelea kustawi na kung’ara katika nyuga mbalimbali.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, Marekani na washirika wake walikuwa na matumaini makubwa watumie machafuko hayo ili wafikie malengo yao, lakini ndoto zao ziliota mbawa baada ya mipango yao kushindwa na kugonga ukuta.

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ambaye alikuwa hapa nchini hivi majuzi amesema hayo baada ya kurejea Lebanon na kubainisha kwamba, hali ya amani na uthabiti nchini Iran iko madhubuti.

Ikumbukwe kuwa mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana, maeneo kadhaa ya Iran yalishuhudia kuanza fujo na ghasia ambapo  katika siku za awali za fujo hizo, ilibainika wazi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya kawaida na vya kisasa vya maadui vilikuwa na mipango maalumu ya uchochezi.

Katika fujo na ghasia hizo ambazo zilibadilika na kuwa ugaidi, watawala wa kisiasa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na vyombo vyao vya habari na halikadhalika vyombo vya habari vinavyopinga Mapinduzi ya Kiislamu vya lugha ya Kifarsi ambavyo vinaungwa mkono na madola ya magharibi na watifaki wao, vilianza kudai kuunga mkono haki za taifa la Iran na kufanya kila lililowezekana kuunga mkono ghasia na kuvuruga usalama wa taifa la Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *