Shirika la kutetea haki za binadamu la Sanad limetangaza kuwa limepokea taarifa zinazoonyesha nia ya Saudi Arabia ya kutekeleza hukumu za kifo kwa idadi ya wafungwa wa itikadi na wanajeshi.
Shirika la hilo la Sanad limeeleza kwenye akaunti yake rasmi ya Twitter kwamba: Mahakama ya kijeshi, ambayo ilianzishwa ili kuwahukumu wafungwa wa kijeshi kutokana na itikadi na mitazamo yao, imetoa hukumu ya kifo dhidi ya makumi kati yao, ambao walihamishiwa kwenye gereza la Al-Ha’ir kutoka mikoa tofauti ya Saudia tangu miezi miwili iliyopita.
Katika ujumbe wake mwingine, shirika la kutetea haki za binadamu la Sanad limethibitisha kuwa miongoni mwa waliohukumiwa kifo ni wafungwa wa kijeshi wa al Huwaitat ambao walikamatwa kwa kutoa maoni yao na kukataa kuhama kwa kulazimishwa. Ripoti zinasema hakuna mawasiliano baina ya wanajeshi hao na familia zao tangu walipohamishiwa kwenye gereza la Al-Ha’ir.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetangaza kuwa linafanya jitihada za kujua majina wanajeshi hao na limetoa wito kwa watu wote huru kufanya jitihada za kukomesha mauaji hayo na kufichua ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Saudi Arabia kote ulimwengu.
Mapema mwezi huu wa Disemba vyombo vya mahakama vya Saudi Arabia vilipitisha hukumu ya kifo kwa vijana kadhaa waliowekwa kizuizini ukiwa ni mwendelezo wa utoaji hukumu za kifo kiholela kwa raia wanaoshikiliwa kwa sababu za kiitikadi.
Wakati vyombo vya habari za Magharibi vimenyamazia kimya matukio hayo, jumuiya za kimataifa zimepaza sauti zao na kutangaza kuwa hukumu za vifo zilizotekelezwa nchini Saudi Arabia katika mwaka huu wa 2022 ni mara mbili zaidi ya mwaka wa 2021.
Kutokana na hali hiyo, timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imeanzisha kampeni ya kutaka kusitishwa mara moja utekelezaji wa hukumu ya kifo nchini Saudia.