Shirika la Ndege la Kenya kuwapiga kalamu marubani waliogoma

Makumi ya maelfu ya wasafiri wa ndani na nje ya nchi wameachwa katika njiapanda katika viwanja vya ndege vya Kenya, baada ya safari zao kukatizwa kutokana na mgomo wa marubani wa Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ).

Zaidi ya wasafiri 15,000 wameathiriwa na mgomo huo uliosimamisha safari zaidi ya 53 za ndani na nje ya nchi, kutokana na mgomo huo ulioanza jana Jumamosi, huku wahudumu wengine wa shirika hilo na wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini Kenya wakijiunga na mgomo huo.

Mikusanyiko ya wasafiri hao waliokanganyikiwa kutokana na mgomo huo ilishuhudiwa jana mchana kutwa na usiku kucha katika Uwanja wa Kimataifa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) na viwanja vingine vya kimataifa vya Mombasa na Kisumu.

Tom Shivo, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa shirika hilo amewataka marubani wanaofanya mgomo kurejea kazini mara moja, vinginenevyo watapigwa kalamu nyekundu.

Chama cha Marubani wa Mashirika ya Ndege ya Kenya (KALPA) kimesema kuwa, wanachama wao hawatarejea kazini hadi matakwa yao yatimizwe. Nao Muungano wa Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege (KAWU) umewataka wanachama wake kujiunga na mgomo huo wa marubani, na wasirejee kazini hadi pale serikali itakapotekeleza makubaliano ya pande mbili yaliyofikiwa mwaka 2019.

Mgomo huo wa marubani unafanyika licha ya mahakama ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuamuru mgomo huo usitishwe, huku viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Uchukuzi, Kipchumba Murkomen wakiwarai marubani hao kurejea kazini na kutafutia ufumbuzi mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo.

Usimamizi wa KQ unasema mgomo huo ni hujuma kwa uchumi wa Kenya, na utalisababishia shirika hilo hasara ya Shilingi milioni 300 za Kenya kila siku.

Kenya Airways inayomilikiwa na serikali ya Kenya ni mojawapo ya mashirika makubwa ya usafiri wa anga barani Afrika, ikiunganisha miji mingi katika mabara ya Afrika, Asia na Ulaya na hivyo mgomo huo umesababisha adha na usumbufu mkubwa kwa wasafiri wengi.

Marubani hao wanataka kubororeshewa mazingira yao ya kazi, sanjari na kurejeshwa michango kwa hazina ya ruzuku ya marubani hao, jambo ambalo usimamizi wa shirika hilo unasisitiza kuwa hauwezekani kwa sasa hadi mwakani 2023.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *