Shirikisho la Soka la Marekani limelazimika kuondoa bendera ya Iran isiyo na nembo halisi ya Jamhuri ya Kiislamu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, na kuweka iliyo sahihi, kufuatia malalamiko ya Tehran.
Katika hatua ya kichokozi na kichochezi, timu ya soka ya wanaume ya Marekani ililiondoa neno ‘Allah’ katika bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa Twitter, kitendo ambacho kimelalamikiwa vikali na viongozi pamoja na wananchi wa Iran.
Iran ilikuwa imeonya kuhusu matokeo mabaya ya kitendo hicho cha Marekani cha kujaribu kubadilisha utambulisho halisi wa bendera ya Jamhuri ya Kiislamu, na ilikuwa inajiandaa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kufuatia uchokozi huo wa Marekani.
Hata hivyo baada ya maonyo makali yaliyotolewa na viongozi na wananchi wa Iran, Shirikisho la Kandanda la Marekani limelazimika kusalimu amri na kuchapisha mitandaoni bendera halisi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ikumbukwe kuwa, Iran imepangwa katika kundi moja na Marekani, pamoja na Uingereza na Wales kwenye fainali za Kombe la Dunia kwenye mpira wa miguu zinazondelea nchini Qatar.
Iran ambayo ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, kesho Jumanne inatazamiwa kucheza na Marekani inayoshika nafasi ya tatu katika mchuano wa kufa kupona katika Uwanja wa Al Thumama.