Kikundi cha mtandao kimechapisha maelfu ya hati na nyaraka za siri za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia.
Serikali ya Saudia, hasa baada ya mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Mohammed bin Salman, kutwaa madaraka, imechukua hatua kali za kuwaandamana waandishi na wanaharakati wa haki za binadamu, makumi ya maulama, waandishi, washairi na wanaharakati wa haki za kiraia na kidini kwa kisingizio cha kuhujumu usalama wa nchi hiyo, na tayari amewahukumu vifungo jela na kuwanyonga baadhi yao.
Televisheni ya Al-Alam imeripoti kuwa, kundi linalojiita Shoka la Ibrahim limechapisha maelfu ya nyaraka za siri za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia, ambazo zina taarifa za maeneo nyeti nchini Saudi Arabia. Pia limechapisha nyaraka zinazohusiana na mamluki wa kigaidi wa utawala wa Saudia.
Kundi hilo la mtandaoni limetishia kutoa nyaraka zaidi kuhusu utawala wa Saudia na kutangaza kwamba, nyaraka hizo ni sehemu ndogo ya nyaraka nyingi zilizodukuliwa za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia.
Wataalamu wanasema, taarifa zilizochapishwa na zitakazochapishwa baadaye, huenda zikaihusisha Saudi Arabia na kashfa nyingi za ukiukaji wa haki za binadamu na jinsi nchi hiyo inavyoyasaidia makundi ya kigaidi duniani.
Maafisa wa serikali ya Saudi Arabia bado hawajachapisha takwimu rasmi kuhusu idadi ya wafungwa wa kisiasa na wa haki za binadamu wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo. Hata hivyo kwa mujibu wa mtandao wa habari ya The Middle East, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuwa idadi ya wafungwa wa kisiasa nchini Saudi Arabia ni karibu watu 30,000, ambao wako katika mazingira magumu, yakiwemo mateso ya kila aina na udhalilishaji.