Siku ya Kimataifa ya Quds na matukio mapya ya kistratijia katika uwanja wa Palestina

Kama dalili zinavyoonyesha, mwaka huu Wapalestina wataadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds kwa msisimko na shauku maalumu. Huenda ni msisimuko na shauku hiyo ndiyo inayapa maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds sifa maalumu na ya kipekee.

Inaonekana kuna mambo kadhaa ambayo yameibua msisimko katika uwanja huo. La kwanza ni kuwa katika miaka ya karibuni maadhimisho ya Siku ya Kiamataifa ya Quds yamekabiliwa na changamoto muhimu kwa kutilia maanani kuwa ulimwengu mzima ulikuwa umekumbwa na tatizo la maambikizi ya corona suala ambalo lilizuia kufanyika maadhimisho hayo kiumati na kijamii. Kwa kuzingatia janga hilo la kiafya duniani, maadhimisho ya Siku ya Quds yaliweza kufanyika tu kupitia mitandao ya kijamii. Kwa kuzingatia hilo na baada ya kupungua maambukizi hayo kutokana na chanjo zilizotolewa pamoja na masuala mengine, mwaka huu kumedhihiri fursa ya kufanyika tena maadhimisho ya siku hiyo muhimu kupitia mikusanyiko ya kijamii na kiumati.

Pamoja na hayo tunapasa kutafuta sababu ya kudhihiri shauku ya kufanyika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika matukio ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na katika maeneo mengine ya Asia Magharibi.

Ndani ya Palestina kwenyewe, stratijia ya makundi ya mapambano ya Kiislamu kwamba haki za Wapalestina zitapatikana tu kupitia mapambano ya silaha imethibiti kivitendo, ambapo utawala haramu wa Israel hata hauuzingatii tena mrengo wa mapatano unaoongozwa na Mahmoud Abbas katika matukio ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hatua ya utawala huo kuupuza mrengo huo na kufungua mlango wa kufanya mapatano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu bila kuushirikisha mrengo wa Mahmoud Abbas inathibitisha wazi kuwa haki za Wapalestina haziweza kupatikana kupitia mapatano bali mapambano. Mrengo wa Mahmoud Abbas haukualikwa kushiriki vikao vyote ambavyo vimeandaliwa kati ya utawala haramu wa Israel na nchi vibaraka za Kiarabu huko Sharm Sheikh, Aqaba na Neqab.

Sula hilo lina umuhimu kwa kutilia maani kuwa kushawishiwa baadhi ya Wapalestina wakubali kufanya mapatano na utawala ghasibu unaokalia ardhi zao kwa mabavu kwa matumaini kwamba wangerejeshewa angalau baadhi ya haki zao, ndoto ambayo haijatimia hadi leo, kumeibua mgawanyiko mkubwa kati ya Wapalestina, na hivyo kuupa utawala huo wa kibaguzi fursa ya kuendeleza siasa zake za ukandamizi dhidi ya Wapalestina kwa kisingizio cha mazungumzo ya amani.

Kwa msingi huo na baada ya kushindwa kabisa mrengo wa mapatano kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mazungumzo na utawala haramu wa Israel, Wapalestina sasa hawana chaguo jingine la kupata haki zao isipokuwa kupitia mapambano ya silaha na utawala huo. Jambo hilo limewapelekea hata wale waliokuwa wakishabikia mazungumzo na utawala wa Israel wafikie ukweli mchungu kuwa hakuna lolote linaloweza kupatikana kupitia mapatano na utawala huo kwa maslahi ya Wapalestina, na ndio maana wameamua kuunga mkono na kushiriki katika mapambano na utawala huo ghasibu.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba kadiri utawala haramu wa Israel unavyohadaa na kuzikaribia zaidi nchi vibaraka za Kiarabu kwa lengo la kuusahaulisha ulimwengu suala la Palestina, ndivyo Wapalestina nao wanavyoimarisha zaidi umoja wao wa ndani na kuunga mkono mapambano kama njia pekee ya kuweza kufikia malengo yao matukufu.

Suala hilo lina umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba kufuatia muamko wa Kiislamu ulioibuka katika nchi kadhaa za Kiarabu miaka iliyopita, baadhi ya nchi za Kiislamu kama vile Uturuki zilijifanya kuwa zinaunga mkono haki na malengo ya Wapalestina na kuwahadaa kuwa zingewasaidia kupigania haki zao, lakini muda haukupita kabla ya sura yao halisi kudhihiri na kubainika kuwa zilikuwa zinatumia vibaya hisia na machungu yao kujinufaisha kisiasa na kiuchumi. Mfano wa hilo ulionekana wazi kuhusiana na Uturuki ambayo ilitumia vibaya machungu na masaibu ya Wapalestina hasa wa kundi la Ikhwan kufikia malengo yake ya Kiothmania mamboleo katika eneo, ambapo leo tunaona kuwa imeimarisha uhusiano wake na tawala za kibaraka kama Saudi Arabia na Imarati ambazo zinahudumia malengo ya Wamagharibi na Wazayuni katika eneo kwa madhara ya Wapalestina.

Hivi sasa ukweli huu umewathibitikia wazi Wapalestina kwamba hakuna rafiki wa dhati anayejali na kutetea maslahi na haki zao kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mrengo wa mapambano. Hilo ni suala jingine ambalo limedhihiri wazi katika matukio ya Palestina ambapo bila shaka litakuwa na taathira muhimu katika maisha ya Wapalestina, na wakati huo huo kuchukuliwa kuwa sifa maalumu katika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *