Leo Jumapili tarehe 13 Rajab mwaka 1441 Hijria sawa na Tarehe 8 mwezi Machi mwaka 2020 ni siku ya kukumbuka kuzaliwa Amirul Muumin Ali (A.S) Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia ulimwenguni.
Ali bin Abi Twalib (as) alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba tarehe 13 Rajab miaka 23 kabla ya Hijra ya Mtume (saw) kuelekea Madina na katika nyakati za utotoni alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu Muhammad (saw). Alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu; na alikuwa msaidizi mkuu wa Mtume Mtukufu (S.A.W) katika marhala zote za tablighi na kueneza mafunzo ya dini ya Uislamu za Mtume wa Uislamu.
Katika Kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa Imam wa Kwanza wa Waislamu Ulimwenguni imepewa jina la “Siku ya Baba.”
Wananchi waumini na wamchao Mwenyezi Mungu wa Iran ya Kiislamu huadhimisha siku hii ya kumbukumbu ya kzualiwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) kwa sherehe mbalimbali kwa kukusanyika katika maeneo matukufu, misikitini na kumbi za masuala ya kijamii.
Shirika la Faraan Swahili linatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu na wapigania ukombozi wote duniani kwa mnasaba huu wa kukumbuka kuzaliwa Amirul Muuminin Ali (as) ambaye alizaliwa msikitini ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, akakulia katika nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na akapigwa upanga akiwa katika ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa Kufa nchini Iraq.