Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, Tehran iko tayari kuchunguza madai ya serikali ya Ukraine kuhusu kutumiwa na Russia ndege zisizo na rubani za Iran katika vita vya Ukraine.
Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana Jumatano baada ya mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus Vladimir Makei.
Katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake huyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kuwa Tehran inakanusha vikali madai kwamba Russia inatumia ndege zisizo na rubani za Iran katika vita ya Ukraine.
Siku ya Jumatatu pia wakati alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia-Pasifiki (OANA), Amir-Abdollahian alisema: “tuko tayari kufanya kikao cha pamoja na Ukraine kuchunguza madai ya uuzaji droni” na akasisitiza kwa kusema: “sisi hatujaipa na wala hatutaipa Russia silaha na ndege yoyote isiyo na rubani ili iitumie katika vita vya Ukarine.” Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alieleza bayana kuwa: “huko nyuma tumepokea silaha mbalimbali kutoka Russia na tungali tunaendelea kupokea; na sisi tunaipatia Russia suhula mbalimbali. Katika vita vya Ukraine, na kwa kuzingatia mtazamo wa msingi wa kupinga vita, tunapinga vita ndani ya Russia na tunapinga ndani ya Ukraine pia na hatujaipatia silaha yoyote ile Russia kwa ajili ya vita vya Ukraine”.
Sisitizo la Iran kwamba haijaipatia silaha Russia kwa ajili ya vita vya Ukraine zikiwemo ndege zisizo na rubani lina umuhimu mkubwa sana kwa kutilia maanani makelele yanayopigwa na Wamagharibi pamoja na serikali ya Ukraine juu ya suala hilo, ambayo bila shaka yanafanywa kwa madhumuni ya kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran. Na hasa baada ya kutangaza kuwa iko tayari kwa ajili ya kuitishwa kikao cha pamoja cha wataalamu wa Iran na Ukraine na kwamba imeshachukua hatua za kivitendo pia juu ya suala hilo. Katika kulitolea ufafanuzi zaidi suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: “tuko tayari timu ya wanajeshi na wataalamu wa Iran na Ukraine wafanye kikao cha pamoja na pia tuko tayari upande wa Ukraine uonyeshe nyaraka zozote ulizonazo; na endapo itatubainikia katika kikao hicho kwamba Russia imetumia ndege isiyo na rubani ya Iran, hatutaliacha hilo vivi hivi”. Amir- Abdollahian aliongezea kwa kusema: “viongozi wa Russia wamesisitiza kuwa silaha zinazotumiwa dhidi ya Ukraine ni za Kirusi; na sisi tuna uhakika kuwa hakuna kitisho chochote kutoka Iran dhidi ya Ukraine na hatujaipa na wala hatutaipa Russia silaha yoyote ile”.
Lakini licha ya Iran kuonyesha msimamo chanya na wa ujengaji, upande wa Ukraine, na bila kuzingatia nia njema hiyo iliyoonyeshwa na upande wa Iran, umekataa kuchukua hatua yoyote chanya, na badala yake ungali umeshikilia madai yake. Madai hayo ya Ukraine yametumiwa na Magharibi kama kisingizio ili kuiwekea Iran vikwazo vipya.
Kwa muda wa siku kadhaa sasa, viongozi wa Ukraine na wa nchi za Magharibi hususan Marekani wamekuwa wakidai kwamba, droni ambazo Russia imezitumia kushambulia miundombinu ya Ukraine zimetengenezwa Iran. Kuhusiana na suala hilo, Alkhamisi iliyopita ya tarehe 20 Oktoba, Umoja wa Ulaya ulitangaza kuiwekea vikwazo vipya Iran kwa kutegemea madai ambayo hayajathibitishwa kuhusu kupatikana nchini Ukraine ndege zisizo na rubani zilizoundwa Iran.
Kabla ya hapo pia Troika ya Ulaya, inayojumuisha Uingereza, Ufaransa na Ujerumani iliuandikia barua Umoja wa Mataifa, iliyokariri madai hayo ambayo hayajathibitishwa kuhusu kutumiwa na Russia droni zilizotengenezwa Iran katika vita vya Ukraine na kuutaka umoja huo ufanye uhakiki ili kubaini kama suala hilo linakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN au la.
Uzushaji makelele na propganda hizo umeandamana na madai ya kuchekesha yaliyotolewa na Marekani dhidi ya Iran. Siku chache zilizopita, Neda Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani alizusha madai mapya dhidi ya Iran na Russia aliposema: “tunaweza kuthibitisha kuwa, askari wa jeshi la Russia walioko Crimea wanaendelea kurusha ndege zisizo na rubani za Iran na wamezitumia kufanyia mashambulio nchini Ukraine”. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshakanusha mara kadhaa madai hayo na kueleza kwamba, hiyo ni sehemu ya vita vya kisaikolojia na kipropaganda vya Magharibi katika muelekeo wa uenezaji chuki na hofu kuhusiana na Iran na kuandaa mazingira ya kuchukua hatua dhidi ya Tehran ikiwemo ya kuiwekea vikwazo vipya. Kwa mtazamo wa Iran madai hayo hayana msingi wowote; na Wamagharibi wamekuwa wakiendesha propaganda katika muelekeo huo kwa uwelewa kamili.
Nukta ya miwsho kabisa hapa ni kwamba, Moscow kwa upande wake, nayo pia imeeleza kinagaubaga kuwa ndege zisizo na rubani zinazotumiwa katika vita vya Ukraine zimetengenezwa Russia. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alipoulizwa, je Russia inatumia droni zilizotengenezwa Iran au la, alisema: “Moscow haina taarifa zozote kuhusu utumiwaji wa droni hizo. Katika vita vya Ukraine zinatumiwa zana za Russia zenye majina ya Kirusi”. Kwa maelezo hayo ni wazi kwamba Wamagharibi wanatafuta kisingizio tu cha kuchukulia hatua dhidi ya Iran; na ili kufikia lengo hilo watatumia kila sababu kuanzia ukiukaji wa haki za binadamu mpaka uuzaji ndege zisizo na rubani kwa Russia..