Sisitizo la kuendelezwa “medani za pamoja za mapambano” na kuangaliwa Israel kama adui wa pamoja wa Wapalestina wote

Huku utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukiwa umeanzisha vita vikali vya kisaikolojia katika siku za hivi karibuni kuulenga uhusiano wa Hamas na Jihadul-Islami, viongozi wa harakati hizo mbili za muqawama za Palestina wamesisitiza katika mazungumzo yao kwamba wameungana na wako kitu kimopja katika mapambano yao dhidi ya utawala huo ghasibu.

Hivi karibuni, utawala wa Kizayuni uliubebesha tena Ukanda wa Gaza vita vingine vya siku tatu ambapo Wapalestina 44 wakiwemo baadhi ya makamanda wa muqawma waliuawa shahidi. Mkakati na stratejia kuu ya utawala haramu wa Israel katika vita hivyo ilikuwa ni kuwalenga makamanda na wanachama wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina. Kwa kutumia stratejia hiyo, dhamira ya adui mzayuni ilikuwa ni kuleta mpasuko kati ya makundi ya Palestina; na hivi sasa angali anaendeleza mkakati huo. Katika siku za karibuni, mtandao wa vyombo vya habari wa Kizayuni umeelekeza nguvu zake zote katika kuchochea mpasuko kati ya Harakati za Hamas na Jihadul Islami na kuvurumiza makombora ya habari za uwongo na uzushi kulenga kamandi ya pamoja ya mirengo ya Muqawama. Anavyoamini adui mzayuni ni kuwa, kwa kutumia siasa za kuzifarakanisha Hamas na Jihadul-Islami ataweza kuudhoofisha Muqawama wa Palestina na kufikia malengo yake maovu dhidi ya Wapalestina.

Katika kukabiliana na mkakati huo mwovu wa utawala wa Kizayuni, makundi na wananchi wa Palestina wamechukua hatua kubwa wakati huu kuliko wakati wowote ule kudhihirisha umoja na mshikamano wao. Kwa kuanzia, harakati za Hamas na Jihadul-Islami zilifanya kikao cha pamoja katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Ujumbe wa Hamas uliowakilishwa na Saleh al Arwari, Naibu Mkuu wa ofisi ya kisiasa pamoja na Halil al Hayyah na Zahir Jabbarin wajumbe wa ofisi ya kisiasa, walikutana na Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina Ziyad, al-Nakhala huko mjini Beirut. Katika kikao chao hicho, harakati hizo za Muqawama, mbali na kusisitizia umoja katika medani za mapambano zilitilia mkazo pia ushirikiano wa kiusalama na kijeshi kwa ajili ya kuzima uchokozi na mashambulio ya kinyama na ya kibaguzi ya utawala haramu wa Kizayuni.

Matunda ya kikao cha Beirut yalikuwa ni kufanikiwa harakati za Hamas na Jihadul-Islami kuzima njama chafu ya utawala ghasibu wa Kizayuni ya kuchochea mifarakano ya ndani katika Ukanda wa Gaza. Kuhusiana na suala hilo, Khalil al Hayyah ambaye ni mkuu wa ofisi ya Hamas ya mahusiano na nchi za Kiarabu na za Kiislamu amesema: “adui yetu ni mmoja na sote tumeungana pamoja kukabiliana naye”. Al Hayyahh ameendelea kubainisha kwa kusema: “kikao cha Jihadul-Islami na Hamas mjini Beirut kilikuwa na maana muhimu, kwa sababu Muqawama ni kitu cha pamoja; na katika kikao hicho tulitilia mkazo kuimarisha kamandi ya operesheni za pamoja.”

Mustafa as-Sawaf, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema hivi kuhusiana na nukta hiyo: “kikao kilichozikutanisha pamoja Hamas na Jihadul-Islami kilikuwa na ulazima na ni jibu la uwongo unaoenezwa na utawala ghasibu. Kikao hicho kinathibitisha umoja kamili uliopo kati ya Hamas na Jihadul-Islami.” Ibrahim al-Mad-hun, mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa yeye anasema: “kikao cha Hamas na Jihadul-Islami hakikuwa kikao cha kawaida, kwani kiliwakutanisha viongozi wa kisiasa, kijeshi na kiusalama na kilikuwa na bishara njema kwa watu wa Palestina ya kwamba, Muqawama umeungana pamoja na uko kitu kimoja katika kushirikiana na kuimarisha muelekeo wao wa pamoja; na kuna hatua za pamoja na mikakati ya kisiasa ambayo inaandaliwa hivi sasa na harakati hizi mbili.”

Sambamba na kikao cha Beirut cha viongozi wa Hamas na Jihadul-Islami, maelfu ya Wapalestina wamefanya maandamano na mikusanyiko ya umma, wakitilia mkazo umoja katika kukabiliana na utawala dhalimu wa Kizayuni. Mikusanyiko hiyo ya Wapalestina ya wananchi na makundi ya Muqawama imefanyika kwa wakati mmoja katika medani na mizunguko mitano ya Gaza, Jenin, Rafah, Damascus na Beirut. Mamia ya viongozi na makundi ya kisiasa na kijeshi ya Palestina pamoja na familia za mashahidi wameshiriki katika mikusanyiko hiyo na wamesisitizia udharura wa Wapalestina wote kuendelea kuonyesha uaminifu na kushikamana na chaguo la Muqawama lililopiganiwa na mashahidi wa Palestina.

Vikao hivyo vya kisiasa na mikusanyiko hiyo ya umma inathibitisha kuwa Wapalestina wanaamini kwa dhati kwamba, umoja ndio siri ya mafanikio ya Palestina katika kukabiliana na utawala ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu; na ni umoja huo ndio unaoutia kiwewe na hofu kubwa utawala huo wa Kizayuni ya kukabiliana na Wapalestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *