Somalia yailalamikia Addis Ababa na kutishia kuwaunga mkono waasi wa Ethiopia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ahmed Moalim Fiqi, amesema iwapo Ethiopia itaendelea mbele na makubaliano yake na kile alichokitaja kuwa waasi wa Somalia, nchi yake itakabiliana nayo kwa njia hiyo hiyo na kuanzisha uhusiano na waasi wa Ethiopia.

Faqi ameongeza kuwa, Ethiopia lazima ijiondoe mara moja kwenye makubaliano yake na eneo la Somaliland yaliyotiwa saini mwanzoni mwa mwaka huu.

Makubaliano hayo yanaipa Ethiopia fursa ya kufika kwenye bandari ya Bahari Nyekundu kwa kukodisha ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 20 mkabala wa kutambua rasmi eneo hilo kama taifa huru.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameongeza kuwa: “Somalia haitaki kuiangamiza Ethiopia, na hilo si kwa maslahi ya Somalia na Pembe ya Afrika kwa ujumla, lakini iwapo uingiliaji kati utaendelea, ina fursa ya kuanzisha uhusiano na waasi wa Ethiopia.”

Faqi ameituhumuu Ethiopia kuwa haitaki kutumia bandari ya Somalia, bali kwa hakika inataka kuchukua sehemu ya ardhi ya Somalia, akibainisha kuwa: “Addis Ababa ilipewa ahadi kutoka Djibouti ya kutumia bandari inayotambuliwa kuwa karibu zaidi na Ethiopia, lakini haikujibu ahadi hiyo, suala ambalo linaonyesha kwamba, inataka kuchukua urithi wa vizazi vijavyo vya Wasomali.”

Itakumukwa kuwa, wiki mbili zilizopita, Ethiopia ilituma mjumbe mpya mwenye cheo cha balozi huko Hargeisa, mji mkuu wa Somaliland, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu kuanza uhusiano kati ya Addis Ababa na eneo hilo lililotangaza kujitenga na Somalia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *