Jumuiya ya shule za Kiislamu nchini Sweden imetangaza kufungwa baadhi ya shule za Kiislamu ambazo baadhi yao ziliasisiwa katika muongo wa 90.
Katika miaka ya karibuni baadhi ya nchi za Ulaya na makundi yenye misimamo mikali yamekuwa yakihujumu Uislamu na matukufu yake katika fremu ya propaganda chafu za kuchafua sura halisi ya dini hiyo na wafuasi wake. Serikali za nchi hizo zinawawekea mashinikizo na kuwanyanyasa Waislamu na dini yao kwa kutumia visingizio mbalimbali.
Tovuti ya habari ya Middle East imeripoti kuwa, serikali ya Sweden tokea mwaka 2019 hadi sasa imefunga shule za Kiislamu 17 na kudai kuwa shule hizo hazifai kwa ajili ya kutoa elimu. Hii ni katika hali ambayo mafunzo ya dini ya Kiislamu ni asilimia tano tu ya elimu ya kawaida inayotolewa mashuleni.
Al Azhar ni moja ya shule 17 kati ya 19 binafsi za Kiislamu za Sweden ambazo zimefungwa tangu mwaka 2019. Wakaguzi wa shule nchini Sweden wameiandikia barua shule ya Al Azhar yenye wanafunzi zaidi ya 200 na kudai kuwa, uongozi wa shule hiyo haufai kuendesha shughuli za utoaji elimu.
Katikati ya mwaka jana wa 2022, Sweden ilichapisha sheria mpya kwa ajili ya taasisi za kidini nchini humo ambazo aghalabu zinatajwa kuwa ngumu, ambazo hata hivyo zimekosolewa na kupingwa na Waislamu nchini humo.
Jamii ya Waislamu, ambayo inaunda asilimia 8 ya wakazi wa Uswidi na aghlabu yao wanatoka Asia Magharibi na Afrika, sasa wanaamini kwamba huenda Sweden isiwe mahali pazuri pa kusomea watoto wao.