Syria yapinga Hatua ya Israel ya kuwafukuza Wapalestina Sheikh Jarrah

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imetoa wito wa kukomeshwa hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuharibu nyumba za Wapalestina na kuwafukuza katika ardhi na makazi yao wakieleza kwamba hatua hiyo ni uhalifu wa kivita.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imetolewa baada ya walowezi wa Kizayuni kuendeleza mashambulia ya mara kwa mara dhidi ya Wapalestina wakazi wa kitongoji cha Sheikh Jarrah katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem) katika siku za hivi karibuni wakisaidiwa ma jeshi la Israel.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imesema katika taarifa yake ya leo Jumanne kwamba, amri ya maafisa wa utawala unaoikalia kwa mabavu Quds ya kuwafukuza Wapalestina katika kitongoji cha Sheikh Jarrah ni jinai ya kivita, kitendo cha kikatili na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu.

Katika taarifa hiyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imezitaka taasisi na mashirika ya kimataifa na ya kibinadamu kuchukua hatua za haraka ili kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kufanya jinai na uhalifu dhidi ya Wapalestina wa Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unawaua shahidi, kuwajeruhi au kuwatia mbaroni wananchi madhulumu wa Palestina kwa visingizio mbalimbali. Wapalestina pia wamekuwa wakifanya operesheni za kulipiza kisasi na kujilinda dhidi ya Wazayuni wakikabiliana na jinai hizo.

Kwa sasa makumi ya familia za Kipalestina zinazoishi katika kitongoji cha Sheikh Jarrah ziko hatarini kuhamishwa kwa nguvu na utawala wa Kizayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *