Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetoa taarifa ambayo sambamba na kulaani vitendo vya vikosi vamizi vya jeshi la Marekani, imetaka kukomeshwa uwepo haramu wa kijeshi wa Washington katika ardhi ya Syria.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema: “Syria inaitaka jamii ya kimataifa izingatie uporaji wa kimpangilio wa maliasili za watu wa Syria unaofanywa na Marekani na vikosi vya wanamgambo wenye uhusiano nayo.”
Katika taarifa yake hiyo, Damascus pia imetaka kurejeshewa maeneo ya machimbo ya mafuta na gesi na fidia kwa rasilimali za nchi hiyo zilizoporwa.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria pia imetoa data na takwimu za hasara iliyopata nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni kutokana na wizi wa mafuta, gesi na madini mengine, pamoja na ngano. Kiasi cha uharibifu huo kimekadiriwa na Syria kuwa ni dola bilioni 19.8. Mbali na hayo, mashambulio ya anga ya mabomu na makombora yaliyofanywa na muungano wa nchi za Magharibi katika maeneo tofauti ya Syria yamesababisha uharibifu na hasara ya dola bilioni 2.9.
Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesisitiza pia: “kimya kinachozidi kuonyeshwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na sera za kichokozi za Marekani na ukiukaji wa misingi ya sheria za kimataifa ni jambo lisilokubalika. Kupuuza mateso wanayopata Wasyria kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya kuna madhara na maafa makubwa kwa maisha ya kila siku ya raia na hakuwaruhusu kupata huduma muhimu na za dharura kama gesi na umeme, hasa wakati wa msimu wa baridi kali”.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria, “mzingiro na hatua za mabavu za nchi za Magharibi dhidi ya Syria ni sawa na uhalifu wa kivita, zimeongeza mateso ya wananchi na kuzorotesha kasi ya mchakato wa ujenzi mpya wa nchi baada ya vita.”
Ikumbukwe kuwa baada ya kushindwa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) likiwa kama tawi la kijeshi la Marekani nchini Syria mnamo Desemba 2016, majeshi ya Marekani yalishika moja kwa moja nafasi ya kundi hilo na kuanza wakati huohuo kuchimba na kuiba mafuta ya Syria.