Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesisitizia ulazima wa vituo vya nyuklia vya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuwa chini ya ukaguzi na usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Bassam al-Sabbagh ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa katika mkutano wa kuupitia upya mkataba wa kupiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT na akabainisha kuwa, vituo na vinu vya nyuklia vya utawala ghasibu wa Kizayuni ni tishio kwa amani na usalama wa eneo la Asia Magharibi na dunia kwa ujumla.
Al-Sabbagh ameongezea kwa kusema, kuhakikisha Asia Magharibi ni eneo lisilo na silaha za nyuklia ni sehemu ya ahadi isiyoweza kutenguliwa ambayo imewekwa na nchi wanachama wa mkataba wa NPT.
Inafaa kuashiria kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio utawala pekee katika eneo la Asia Magharibi unaomiliki silaha za nyuklia; na kwa uungaji mkono unaopata kwa Marekani hadi sasa umekataa mpango wake wa silaha za nyuklia kufanyiwa ukaguzi na kuwa chini ya usimamizi wa kimataifa.
Imekuwa ikikadiriwa kuwa utawala haramu wa Israel unamiliki vichwa kati ya100 hadi 200 vya atomiki. Hata hivyo wataalamu wa masuala ya nyuklia wanaeleza kwamba; hadi sasa kiwango hicho kitakuwa kimeshaongezeka mara mbili.
Alipohutubia siku ya Jumanne katika ufunguzi wa mkutano huo wa kupitia upya mkataba wa NPT, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitahadharisha juu ya hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani.
Guterres alitoa indhari kwa nchi wanachama wa NPT kwamba dunia inakabiliwa na hatari ya kutokea vita vya nyuklia ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu zama ambapo Vita Baridi vilikuwa vimefikia kilele na kwamba kosa moja tu la kimahesabu litakalofanywa litapelekea kutokea maangamizi ya kinyuklia.
Katibu Mkuu wa UN aligusia vita vilivyoanzishwa na Russia nchini Ukraine na mivutano inayoendelea katika Peninsula ya Korea na Asia Magharibi na akasema: “kuangamiza silaha za nyuklia ndilo litakuwa hakikisho pekee la kutotumiwa silaha hizi”.