Taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu; mzongano usiozongoka wa uzushaji tuhuma dhidi ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani taarifa ya hivi karibuni ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya ile inayojiita kamati ya pande nne na kusisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na Iran kuhusiana na visiwa vyake vitatu zinalenga kulinda mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya taifa hili.

Nasser Kanaani, ametoa jibu kwa vipengee vya taarifa ya kikao cha 158 cha  mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya ile inayojiita kamati ya pande nne kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: kutolewa taarifa kama hizo ni ishara ya kutokuwa na ufahamu sahihi baadhi ya nchi zilizotajwa kuhusiana na mwenendo wa matukio yanayojiri katika eneo na kujifanya hazijui ukweli halisi wa hali ya eneo la Asia Magharibi.

Mbali na watoaji wa taarifa hiyo kurudia madai ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) kuhusu visiwa vitatu vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bumousa, pamoja na madai kwamba Iran inaingilia masuala ya Yemen, wametaka pia washirikishwe kwenye mazungumzo ya nyuklia na kuongezwa mpango wa makombora wa Iran kwenye ajenda za mazungumzo hayo.

Licha ya nyaraka sahihi kuthibitisha kwamba visiwa hivyo vitatu vya Tomb Kubwa,Tomb Ndogo na Bumousa ni mali ya Iran, lakini imekuwa ni kawaida, wakati tawala za Kiarabu zinapokutana katika vikao kama hivyo, -na bila shaka kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni-, kuibua mjadala wa kudai kwamba Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati ndio mmiliki wa visiwa hivyo; hali inayoashiria mwendelezo wa  mzongano usiozongoka wa uzushaji tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutobadilika tabia na mwenendo wa tawala hizo.

Katika ramani ya Jeshi la Wanamaji la Uingereza ya mwaka 1881, ramani ya Wizara ya Masuala ya Bahari ya Uingereza ya mwaka 1863, na vilevile ramani ya Iran iliyochorwa na Wizara ya Vita ya Uingereza mnamo mwaka 1886, visiwa hivyo vitatu vimepakwa rangi ya ardhi ya Iran; na hivyo ni miongoni mwa vielelezo vya hati na nyaraka za kimataifa zilizopo zinazothibitsiha mamlaka ya utawala ya Iran kwa visiwa hivyo. Sambamba na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kila mara kwamba visiwa vya Iran vya Bumousa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya Iran; kwa hivyo utoaji wa taarifa kama hizo hautabadilisha chochote juu ya suala hilo.

Nukta ya kuzingatiwa ni kwamba, taarifa ya hivi karibuni ya nchi za Kiarabu imetolewa, ilhali katika miezi ya karibuni, baadhi ya nchi hizo zimeanza kuchukua hatua nzuri na za maelewano kwa lengo la kuboresha uhusiano wao na Iran. Baada ya Kuwait, Muungano wa Falme za Kiarabu ulikuwa nchi ya pili kutangaza kwamba utatuma balozi wake mjini Tehran. Saudi Arabia, ambayo ndiye msababishaji mkuu wa kupooza uhusiano wa tawala za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na Tehran, hivi sasa inaendelea kufanya mazungumzo na Iran kwa upatanishi wa Iraq, na imeelezea kuridhishwa na mchakato wa mazungumzo hayo. Kwa hivyo, madai na tuhuma za kila mara zilizotolewa katika taarifa ya karibuni ya kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inachukuliwa kuwa ni mwenendo wenye sura ya mgongano na mkinzano, ambao hausaidii kupunguza mivutano na kuimarisha maelewano katika ukanda huu.

Taarifa ya hivi karibuni ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu vilevile imekariri kwa mara nyingine tena madai kwamba Iran inaingilia masuala ya ndani ya Yemen, jambo ambalo lina mgongano wa wazi na uhalisia wa mambo. Muelekeo endelevu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na mgogoro wa Yemen daima umekuwa ni wa kuunga mkono suluhu ya kisiasa kwa ajili ya kukomesha vita nchini humo. Ukweli ni kwamba baadhi ya nchi za Kiarabu kama Imarati, ni mmoja wa wasabibashaji wakuu wa mgogoro wa sasa wa Yemen kutokana na msimamo wake wa kuifuata Saudi Arabia katika kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo, ambayo yamefanyika kwa uungaji mkono na Marekani; na kwa hivyo kujitoa kwake kimasomaso kwa kutaka kuwabebesha lawama wasiohusika, hakuipunguzii dhima iliyonayo ya kufidia hasara ilizosababisha katika mgogoro huo.

Ni dhahiri kuwa, kipaumbele cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan serikali ya 13 ni kuimarisha ushirikiano na kustawisha uhusiano na majirani zake wote zikiwemo nchi za mpaka wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi; lakini kwa upande wao, nchi hizo zinapaswa zifahamu kwamba, matakwa yao yasiyokubalika na kukariri tuhuma za uwongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sio suluhisho la matatizo ya eneo hili wala ya na nchi hizo, bali ukweli ni kwamba, yanazidi kuchochea hali ya kutoaminiana kati ya majirani.

Msemaji wa chombo kikuu cha diplomasia cha Iran amesisitiza pia kwamba, msimamo wa kila mara wa Iran ni kuwaalika majirani zake kwa mazungumzo na kuondoa sutafahamu zilizopo kwa njia za kidiplomasia; na akawashauri mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwamba, badala ya nchi hizo kurudia tuhuma za kila mara na zisizo na maana, zijikite kushughulikia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *