Mashirika na taasisi za haki za binadamu za kimataifa zaidi ya 170 zimetaka kuhitimishwa maafa ya binadamu huko Yemen na mzingiro dhidi ya nchi hiyo.
Kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya nchi kavu, baharini na angani. Hadi sasa Wayemeni elfu 11 wameuliwa katika vita hivyo tajwa huku watoto zaidi ya milioni mbili wakisumbuliwa na utapiamlo. Wakati huo huo raia wa Yemen zaidi ya milioni 17 wakiwemo watoto milioni 9 wanakabiliwa na uhaba wa maji, huduma za afya na tiba nchini humo.
Mashirika na taasisi 172 za kutetea haki za binadamu za kimataifa leo yametoa taarifa yakieleza wasiwasi wao mkubwa kufuatia hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili wananchi wa Yemen na kutangaza kuwa: maafa hayo ya binadamu yamesababisha Wayemeni zaidi ya milioni 20 kukabiliwa na njaa na hatari ya kifo, na kwamba idadi ya waathirika inaongezeka siku baada ya siku.
Taarifa ya mashirika hayo ya kimataifa imeongeza kuwa, maafa hayo ya binadamu yanaendelea kuwakumba wananchi wa Yemen sambamba na kukatwa mishahara ya wafanyakazi na kuendelezwa vikwazo dhidi ya bandari na viwanja vya ndege nchini humo.
Katika taarifa yao hiyo, mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yamezitaka nchi waitifaki katika muungano vamizi dhidi ya Yemen kulipa haraka mishahara ya wafanyakazi wa mikoa yote na kuondoa vikwazo dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana’a na bandari ya al Hudaidah.