Jarida la Express limemnukuu mtaalamu wa ngazi ya juu katika sekta ya afya na kuripoti juu ya uwezekano wa kuibuka maambukizi ya wimbi jipya la spishi inayoibukia ya Corona huko Uingereza.
Hadi sasa watu 213,000 wameaga dunia nchini Uingereza baada ya kuambukizwa aina mbalimbali za spishi za kirusi cha corona tangu wimbi hilo la maradhi liikumbe nchi hiyo mwaka 2019.
Stephen Griffin mtaalamu wa Akademia ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Leeds ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuibuka wimbi jipya la maambukizi ya corona ambayo yamekuwa yakienea Uingereza tangu mwezi Oktoba mwaka huu na kueleza kuwa: kuna wasiwasi kwa kuzingatia aina hii ya maamabukizi ya corona, pamoja na kinga iliyopungua ya wale ambao wamechanjwa kwa muda mrefu na kuongezeka kwa idadi ya watu walioambukizwa na ugonjwa
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuanzia mwezi Oktoba hadi sasa, kila siku mtu mmoja huripotiwa kuambukizwa spishi hiyo ya corona kati ya kila watu 45. Griffin ametahadharisha kuhusu kupungua kwa kinga za mwili miongoni mwa watu kutokana na kuwepo mwanya mkubwa baina ya upigaji chanjo na kuitaja spishi hiyo mpya ya kirusi cha corona kuwa changamoto kwa viongozi wa sekta ya afya ya Uingereza.
Hii ni katika hali ambayo, vituo vya huduma za afya na hospitali nchini Uingereza zimelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa kutokana na mgomo mkuwa wa wauguzi na wafanyakazi wa kitengo cha magari ya kubebea wagonjwa. Wimbi jipya la maambukizi ya corona linatazamiwa kulemaza mfumo wa afya wa Uingereza.