Takriban wanawake 50 waliotekwa nyara nchini Burkina Faso wapatikana

Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, takriban wanawake 50 waliotekwa nyara hivi majuzi kaskazini mwa Burkina Faso na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi, wamepatikana.

Shirika la habari la Burkina Faso limeripoti habari hiyo kwa kuandika: “Wanawake waliotekwa nyara na magaidi usiku wa tarehe 12-13 mwezi huu wa Januari 2023 huko Arbinda wamepatikana.”

Shirika la Habari la Taifa pia limesema, limenukuu habari hiyo kutoka kwa “vyanzo vya kuaminika” lakini halikusema ni vyombo gani hivyo.

Gavana wa eneo la Sahel, Rodolphe Sorgho amesema kuwa, vikundi vya kigaidi vilivyojizatiti kwa silaha viliwateka nyara wanawake na wasichana waliokuwa wakitafuta matunda mwituni. Baada ya kutekwa nyara, mwendesha mashtaka wa jimbo la kaskazini la Djibo, Issouf Ouedraogo, aliripoti kuwa wasichana na watoto wachanga walikuwa miongoni mwa waliotekwa nyara.

Chama cha Burkinabe Movement for Human and People’s Rights na duru nyingine ziliripoti kuwa, takriban wanawake 61 walitekwa nyara, wakiwemo wenye umri wa chini ya miaka 18. Wananchi wa Burkina Faso wamekumbwa na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya kigaidi tangu mwaka wa 2015. Maelfu ya shule zimefungwa, maelfu wameuawa na mamilioni ya wengine wamehama maeneo yao.

Kwa upoande wao, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres walilaani vikali kutekwa nyara zaidi ya wanawake na wasichana 50 nchini Burkina Faso na kuitaka serikali ya nchi hiyo iwasake, iwakomboe na itoe adhabu kali kwa waliowateka nyara wanawake na wasichana hao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *